Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe.Prof. Adolf Mkenda amesema Serikali ya awamu ya Sita inaendelea kufanya mageuzi makubwa katika sekta ya elimu ikiwemo kuandaa walimu watakaokidhi soko la ajira wanaosoma katika vyuo 35 vya ualimu vilivyopo nchini.
Pia Serikali inaendelea kuboresha mazingira ya ujifunzaji na ufundishaji katika ngazi zote za elimu kuanzia Msingi, Sekondari, Vyuo vya kati na Elimu ya juu ili kuleta tija kwa wahitimu wawapo katika soko la ajira.
Mhe.Prof.Mkenda amebainisha hayo leo Aprili 25,2023 jijini Mwanza wakati akizungumza na wadau wa elimu kabla hajazindua mradi wa ujenzi wa jengo la Maktaba na Maabara za Sayansi na Tehama katika Chuo cha Ualimu nchini ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 59 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
"Maelekezo ya Mhe. Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.Samia Suluhu Hassan ni kwamba wanafunzi wakihitimu waweze kujiajiri anachotaka ni elimu yetu hapa nchini iongeze ujuzi kwa vitendo," amesema Mhe.Prof.Mkenda.
Akizungumzia miaka 59 ya Muungno wa Tanganyika na Zanzibar itakayoadhimishwa kesho April 26 2023, Prof.Mkenda amewaasa vijana wanaosoma vyuoni wasimamie muungano huo bila kuyumba, kutetereka na kubabaika ili kuwaenzi waasisi wa nchi hii.
"Chuo hiki kimeanza mwaka 1939 hadi leo vijana kutoka sehemu balimbali nchini wanakuja hapa kusoma hii ni kutokana na amani na utulivu iliyopo katika nchi yetu ambayo ni matunda ya waasisi wa nchi hii hivyo tusimame kidete kuutetea na kuulinda kwa kila hali muingano wetu,"
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe.Adam Malima amesema kwa kipindi cha mwaka 2020/2021 na 2021/2022 Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.Samia Suluhu Hassan imeimarisha Elimu ya Ualimu kwa kupeleka fedha katika vyuo vya Ualimu kwa ajili ya mafunzo ya walimu tarajali na mafunzo kazini kwa watumishi.
"Kupitia uimarishaji huo Chuo cha Ualimu Butimba kwa kipindi cha mwaka 2020/2021 na 2021/2022 kilipokea zaidi ya Sh bilioni moja kwa ajili ya Ujenzi wa Maabara za Fizikia, Kemia Maabara ya Tehama, Vyumba vinne vya madarasa, Ukumbi wa mihadhara na kukarabati majengo ya Maabara ya Baiolojia na Maktaba.
"Pia katika kipindi cha mwaka 2021/2022 na 2022/2023 Serikali ya awamu ya sita ilileta fedha katika chuo hiki kiasi cha Sh milioni 715,163,287.28 kwa ajili ya kugharamia Mafunzo ya Ualimu kwa vitendo, mafunzo hayo hutoa fursa kwa wa wanachuo kupata tajiriba ya kumudu Maisha ya kazi na uhalisia wa Mazingira ya kazi, " amesema Mhe.Malima na kuongeza
"Pamoja na kujenga majengo ya miundombinu ya Chuo Kipya cha Murutunguru kilichopo Wilaya ya Ukerewe Mkoani Mwanza kwa kipindi cha mwaka 2020/2021 hadi 2023 Serikali imepeleka fedha zaidi ya Sh milioni 369 kwa ajili ya kujenga bweni la wasichana lenye uwezo wa kuhudumia watumiaji 80 na vyumba vinne vya madarasa vyenye uwezo wa kuhudumia watumiaji 200 kwa wakati mmoja," ameeleza Mhe.Malima.
Akisoma taarifa ya mradi wa Ujenzi na Ukarabati wa Majengo ya Maabara za Sayansi, Tehama na Maktaba kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Prof.Carolyne Nombo, Mkurugenzi Msaidizi Ualimu wa Wizira hiyo, Bwana Huruma Mageni amesema mradi huo umetekelezwa kupitia mradi wa kuendeleza Elimu ya Ualimu (TESP) kwa gharama ya Sh Milioni 467,695,598.00.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.