SERIKALI YAANIKA TAKWIMU ZA MAENDELEO YA UTUMISHI YALIYOPATIKANA MWANZA
Serikali mkoani Mwanza imesema Katika kipindi cha mwaka 2023/2024 na 2024/2025 Sekretarieti ya Mkoa na Halmashauri zake nane zimepata mafanikio makubwa katika kuhakikisha kwamba masuala ambayo ni kero kubwa kwa watumishi yamefanyiwa kazi kwa kiasi kikubwa.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda katika Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi duniani yaliyofanyika Kimkoa katika Viwanja vya KWIDECO Wilayani Kwimba ambapo amesema Serikali imelipa watumishi 3,556 fedha za malimbikizo ya mishahara (Salary Arreas) yenye jumla ya shilingi 6,896,355,330/= na Watumishi wapya 831 wameajiriwa ili kupunguzia mzigo kwa watumishi.
Aidha, Mkuu wa Mkoa amesema Serikali imelipa madai ya watumishi 4,015 yasiyo ya mshahara (mfano likizo, matibabu uhamisho n.k) yenye kiasi cha Shilingi 3,283,016,595,486/=.
“Si hayo tu bali pia Watumishi 9,829 wa kada mbalimbali wamepandishwa madaraja (vyeo) kwa mwaka wa fedha 2023/2024 na watumishi 601 wamebadilishiwa kada (Recategorization) kwa mwaka wa fedha 2023/2024”.
Kadhalika Watumishi wameendelea kupewa fursa za kujiendeleza ambapo hadi kufikia mwezi Aprili, 2025 jumla ya watumishi 528 wapo masomoni katika Vyuo mbalimbali. Watumishi 1,352 wameajiriwa katika sekta mbalimbali ndani ya Mkoa wa Mwanza. Amesema Mhe. Mtanda akiendelea kuelezea mafanikio hayo.
Mkuu wa Mkoa ameendelea kwa kusema Utekelezaji wa Mfumo wa Usimamizi wa Utendaji Kazi katika Utumishi wa Umma (PEPMIS) kwa mwaka wa fedha 2024/2025, umefikia asilimia 59.72 huku Mfumo huo ukiwa na lengo la kuimarisha uwajibikaji na utendaji kazi unaojali matokeo katika Utumishi wa Umma ili kuwaletea wananchi maendeleo.
Kuhusu suala ya Ajira kwa Vijana Mkuu wa Mkoa amesema Jumla vikundi 37 vya vijana hadi sasa vimewezeshwa miundombinu ili kufuga Samaki kwenye vizimba 161 ndani ya ziwa Victoria hivyo
kupunguza changamoto ya ajira kwa vijana wa Mkoa wa Mwanza.
“Miradi ya Kimkakati imezalisha ajira mbalimbali kama vile Ujenzi wa madarasa na ujenzi wa miundombinu mingine ya Utawala, Elimu na Afya ulizalisha ajira 15,855, Ujenzi wa Meli Mpya ya MV Mwanza Hapa Kazi tu umezalisha ajira 1,000, Ujenzi wa Reli ya Kisasa ya SGR umezalisha ajira 3,075, Ujenzi wa daraja la JPM umezalisha ajira 1,875 Huku Ajira 2,758 zimezalishwa kupitia fedha za Mfuko wa Vijana, Wanawake na Watu wenye Ulememavu.”.
Mkuu wa Mkoa amesema kwa kufafanua mafanikio hayo ni kuwafanya Wafanyakazi hao waweze kupata picha halisi ya mafanikio makubwa na ya kupigiwa mfano yaliyopatikana kwenye upande wa watumishi katika Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.