Serikali imetoa maazimio 14 kwa walimu wakuu, maofisa elimu wa kata na taaluma ambayo wanapaswa kuyatekeleza kiukamilifu kwa lengo la kuinua ufaulu kwa shule za msingi 2019/2020.
Maazimio hayo yalifikiwa katika kikao kilichofanyika jijini Mwanza kati ya Afisa elimu mkoa na wakuu wa shule, maafisa elimu kata na taaluma ambapo ilibainika zaidi ya wanafunzi 1,034 hawakufanya mtihani wa ukamilifu ‘mock’ ngazi ya mkoa, idadi ambayo ilielezwa ni kubwa sana.
Akizungumza na waandishi wa habari, Afisa Elimu Mkoa wa Mwanza, Michael Ligola alisema katika majadiliano ya pamoja wamebaini sababu kadhaa ambazo kwa namna moja au nyingine zinashusha taaluma na ufaulu.
Alisema kutokana sababu hizo, kama Serikali ya mkoa imeelekeza walimu wakuu, maafisa elimu kata na taaluma kutekelezwa maazimio 14 kuanzia sasa na matokeo yake yatapimwa kuanzia ufaulu wa mtihani wa kuhitimu darasa la saba 2019.
“kwanza tumewataka walimu wakuu kuacha migogoro na walimu wengine, pia wanapaswa kukaa na wazazi ili kurahisisha utendaji kazi, walimu wakuu kutoa motisha kwa walimu wanaojituma na bidii zao zinaonekana. Walimu wakuu waipende kazi yao na kuongeza juhudi na maarifa ya usimamizi na ufuatiliaji taaluma.
“maofisa elimu kata na walimu wakuu kuhakikisha wanashirikiana na watendaji wa kata na vijiji kuthibiti utoro, kuongeza utoaji wa majaribio darasani kwa kutumia mitihani iliyopita, kuhamasisha wanafunzi wapate chakula shuleni.
“Walimu wakuu kutambua watoto wenye uwezo mdogo katika somo la hisabati na kuwasaidia maswali kuazia swali la 1-25 kwa vitendo, walimu bingwa kuongeza bidii katika darasa la saba, kuanziasha ufundishaji shirikishi kwa kujadiliana mada ngumu ili kuongeza uelewa, mwalimu mkuu kupunguza safari na vikao nje ya kituo cha kazi,”alisema.
Ligola alisema maazimio mengine ni walimu wakuu kuhimiza ufundishaji wa kusoma, kuhesabu na kuandika (K.K.K) katika darasa la kwanza na la pili, walimu kuwa na upendo kwa wanafunzi na kuwajenga kisaikolojia kwa kuwaondoa woga, wazazi waelimishwe umuhimu wa kusomesha watoto wa kike na sio kuwafanya kama kitega uchumi.
Wakati wa ufunguzi wa kikao hicho, iligundulika wanafunzi 1,034 hawakuonekana katika vyumba vya mtihani wa ukamilifu mock’ mkoani Mwanza.Pia kikao hicho kilikusudia kupata majibu kutoka kwa maafisa elimu na wakuu wa shule sababu ya baadhi ya halmashauri kutofikia asilimia 90 ya ufaulu ambao ni lengo la mkoa huo.
Kwa mujibu wa takwimu za mkoa huo zinaonyesha halmashauri ya Ilemela ilifikia asilimia 98.3, Sengerema 97.1, Misungwi 96.6, Jiji la Mwanza 95.2, Magu 92, Ukerewe 85.4, Kwimba 84.6 na Buchosa 80.5.
Ligola alisema lengo ni kuona kuweka mikakati na kutatua changamoto zilizopo ili kila halmashauri iweze kufikia asilimia 90 ya ufaulu katika mitihani ya kitaifa. Ligola alisema Julai 17-18 mwaka huu kulifanyika mtihani wa mjaribio mkoa ambapo wanafunzi 68,356 kutoka shule za msingi 944 walitarajiwa kufanya lakini waliongia vyumbani siku hiyo ni 67,322 kati ya hao wavulana 31,789 mna wasichana 35,533 na asilimia 98.3.
Alisema wanafunzi ambao hawakufanya mtihani huo 1,034 kati ya hao wavulana ni 347 na wasichana 687 sawa na silimia 1.5, hivyo alisema kiwango hicho cha wanafunzi wasiofanya mtihani ni kikubwa na kinapaswa kutafutiwa suluhisho.
“Lengo la Serikali ni ufaulu uwe asilimia 100 kitaifa lakini hapa Mkoa wa Mwanza tulijiwekea malengo yetu yawe asilimia 90 au zaidi,sasa katika mitihani ya majaribio tuliyofanya ngazi ya mkoa baadhi ya halmashauri zimeonekana kutofikia lengo letu, sasa nimelazimika kuwakutanisha ili kila mmoja aseme kilichomkwamisha hali hiyo kujitokeza.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.