Serikali kwa kushirikiana na Shirika lisilo la Kiserikali la Jhpiego imeendelea kuboresha huduma za matibabu ya saratani ya matiti Mkoani Mwanza kupitia Mradi wake wa Beat Breast Cancer awamu ya pili unaodhaminiwa na PFIZER Foundation ambao unalenga kupunguza vifo vinavyotokana na ugonjwa huo kwa kuimarisha uchunguzi wa mapema na upatikanaji wa matibabu.
Akizungumza leo Oktoba 22, 2025 na waandishi wa habari ofisini kwake, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Dkt. Jesca Lebba ameipongeza serikali kwa hatua hiyo muhimu na kuishukuru kwa kuuchagua Mkoa wa Mwanza kuwa miongoni mwa wanufaika wa awamu ya pili ya mradi huo.
Dkt. Lebba amewataka wananchi wa Mkoa wa Mwanza kuchangamka kwa kujitokeza kwa wingi katika vituo vya kutolea huduma za afya ili waweze kuchunguza afya zao na kupatiwa matibabu.

“Tutahakikisha tunawafikia wananchi wa maeneo yote na nitoe rai kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kuja kuchunguza afya zao na kupatiwa huduma za uchunguzi, ushauri na matibabu”.
Ameongeza kuwa changamoto kubwa ambayo wanakutana nayo ni uelewa mdogo wa jamii juu ya dalili na matibabu ya saratani ya matiti, watoa huduma wachache pamoja na vituo vya kutolea huduma hiyo ya vipimo na elimu juu ya ugonjwa huo.
Aidha, amesema wameweza kufanya uchunguzi kwa wanawake zaidi ya 23,000 na kuanzia mwezi Januari mpaka Septemba mwaka huu wananchi 46 wamebainika kuwa na saratani ya matiti na kati yao 27 wameshaanza kupatiwa matibabu na wengine wapo katika ushauri nasaha.
Naye Daktari Bingwa wa Upasuaji kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Sekou-Toure Dkt. Jackson Chiwaligo amewasisitiza wanawake kujifanyia uchunguzi wa awali ili waweze kutambua mabadiliko katika miili yao, huku akitoa wito waweze kufika hospitali pale ambapo watahisi mabadiliko yoyote katika matiti.

Mkoa wa Mwanza ni miongoni mwa Mikoa minne kwa Tanzania bara ambayo inanufaika na mradi wa PFIZER-BREAST CANCER na kutoa huduma ya kupima na kutibu saratani ya matiti ukiwa na vituo 32 zikiwemo Hospitali ya Kanda, Hospitali ya Rufaa, Hospitali za Wilaya na Halmashauri huku ikifanikisha kutoa elimu kwa watoa huduma 60.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.