Serikali imetenga Sh bilioni 5.9 katika mwaka huu wa fedha ambazo zitatumika katika kuajiri ajira mpya, kulipa mishahara ya watumishi sanjari na uboreshaji wa shughuli za Kampuni ya Huduma za Meli Nchini ( MSCL).
Hayo yamesemwa mwishoni mwa wiki jijini hapa na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwele wakati wa ziara yake ya kikazi ambapo alipata fursa ya kutembelea ujenzi wa mradi wa chelezo, eneo ambalo litatumika kuunda meli mpya iliyoahidiwa na Rais John Magufuli kwa ajili ya wakazi wa mikoa ya Kanda ya ziwa na kukagua ukarabati unaoendelea wa meli za MV Victoria na MV Butiama.
Alisema lengo la serikali kutoa kiasi hicho cha fedha ni kuiwezesha Kampuni hiyo ya huduma za meli ya serikali kutekeleza majukumu yake ya kutoa huduma za usafirishaji wa majini sayansi na pia kuondokana na changamoto za muda mrefu ambazo zilikuwa ni kikwazo katika kipindi cha miezi 27 ili baadaye iweze kujitegemea na kutoa gawio la fedha serikalini.
Alisema kabla ya kutoa fedha hizo, tayari serikali kupitia kwa Rais Dk. John Magufuli alitoa kiasi cha Sh bilioni 2.1 kwa ajili ya kuwalipa watumishi waliokuwa wamekaa muda mrefu bila ya kulipwa mishahara yao na kuifanya MSCL kuendelea kuwa chombo imara zaidi katika utekelezaji wa majukumu yake.
“ Nitumie fursa hii kuwaeleza wananchi kwamba serikali imeyamaliza matatizo yaliyokuwa yanaikabili MSCL na sasa inakwenda kutekeleza majukumu yake vyema,” alisema.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa MSCL Mhandisi Erick. B. Hamissi alimshukuru Rais John Magufuli kwa kutoa fedha ambazo sasa zinaweza kuondoa changamoto ambazo kwa muda mrefu zimekuwa zinaikabili kampuni ya MSCL.
Alisema Rais John Magufuli ameonyesha kuwa ana nia njema na MSCL na wakazi wa mikoa ya Kanda ya Ziwa kwa kuiwezesha MSCL na kuhakikisha huduma za usafiri wa majini zinaaimarika kwa manufaa mapana ya kuimarisha uchumi wa kanda ya ziwa na taifa kwa ujumla.
Alisema kwa muda wowote sasa serikali kupitia MSCL inatarajia kusaini mkataba mwingine wa ujenzi wa meli mpya katika Ziwa Tanganyika itakayokuwa na uwezo wa kubeba abiria 600 na tani 400 za mizigo , ukarabati wa meli ya Mv Liemba iliyo katika Ziwa Tanganyika na ukarabati wa meli za Mv Umoja na Mv Serengeti ambazo zitakapokamilika zitaanza kufanya shughuli za usafirishaji katika Ziwa Victoria.
Alisema miradi hiyo minne ambayo haijsainiwa, ikiwemo ujenzi wa meli mpya na ukarabati wa meli hizo ( MV Liemba, MV Umoja na MV Serengeti-Ziwa Victoria, alisema tayari MSCL imeishamaliza taratibu zote za manunuzi na kuandaliwa mikataba na kwamba taratibu zote za kusainiwa kwa mikataba hiyo zinaendelea kukamilishwa.
Aidha alisema kuwa serikali pia imetenga kiasi cha fedha Sh bilioni 70 katika mwaka ujao wa fedha kwa ajili ya ujenzi wa meli mpya za mizigo zinazotarajia kufanya huduma ya usafirishaji katika Ziwa Tanganyika na Victoria ambapo fedha hizo pia zitatumika kwenye ukarabati wa mkubwa wa meli ya Mt Sangara iliyoko Ziwa Tanganyika.
“Kwa sasa hatujapata wakandarasi na kwenye mradi hiyo kwa sasa tuko kwenye hatua ya manunuzi,” alisema Hamissi.
Alisema mikakati ya MSCL ni kutekeleza Rasimu ya Mpango Mkakati wa muda mrefu kuanzia 2019-2025, hii ikiwa ni pamoja na kuongeza idadi ya meli za kusafirisha mabehewa ndani ya Ziwa Victoria, kujenga meli kubwa ya kubeba mafuta katika ziwa Tanganyika, kujenga meli kubwa ya kubeba mizigo hususani makontena katika Ziwa Tanganyika na Victoria.
“ Hii ni pamoja na kuhakikisha ukarabati wa meli za MV Victoria na Butiama na ujenzi wa cherezo unakamilika ndani ya muda uliopangwa ili kuruhusu ujenzi wa meli mpya katika ziwa Victoria ambayo ni ahadi ya Mheshimiwa Rais kutekelezwa kama ilivyopangwa,” alisema Hamissi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.