Serikali imenunua injini mbili mpya kwa ajili ya kuzifunga katika Kivuko cha MV Nyerere kinachotoa huduma kati ya Bugorola na Ukara katika Wilaya ya Ukerewe Mkoani Mwanza ili kuongeza ufanisi zaidi.
Kauli hiyo imetolewa na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (Temesa), Dk. Mussa Mgwatu wakati akizungumza na waandishi wa habari alipotembelea kivuko hicho ambao alisema injini hizo mbili mpya zina thamani ya Sh milioni 191.
Alisema kivuko hicho tangu kianze kufanya kazi mwaka 2004 eneo hilo hakijawahi kufanyiwa ukarabati mkubwa kitendo ambacho kimepunguza ufanisi wa kazi ambapo aliwaagiza mafundi wanaofunga injini hizo wafanye kazi usiku na mchana ili waweze kukamilisha ufungaji huo mapema iwezekanavyo ili kivuko kiendelee kutoa huduma ya usafrishaji wa abiria na mali zao.
Aliongeza kuwa Serikali imedhamiria kuimarisha usafiri wa vivuko katika Ziwa Viktoria kwa kujenga vivuko vipya vitakavyotoa huduma katika maeneo mbalimbali yakiwemo ya Kigongo, Busisi, Kayenze, Bezi, Chato, Bwina, Bukondo, Senga, Muharamba, Kikumbaitale, Izumacheli na Nkome pamoja na kuvifanyia ukarabati vivuko vya MV. Nyerere, MV. Misungwi, MV. Sengerema na MV. Sabasaba.
“Katika kivuko hiki cha MV Nyerere naomba nitoe maagizo kwa mafundi wanaofunga injini hizo, wafanye kazi usiku na mchana ili kukamlisha kazi hiyo mapema na huduma ziweze kuendelea kwa wananchi wa maeneo haya, viongozi naombeni kuwa karibu na mafundi hao,”alisema Dkt. Mgwatu.
Naye Meneja wa Vivuko Temesa, Mhandisi Hassan Karonda alisema mifumo ya injini ya kivuko cha MV Nyerere imechoka sana kwa sasa kwa kuwa ni ya muda mrefu.
Alisema injini mbili mpya pamoja na giaboksi zinazofungwa katika kivuko hicho ni za aina ya perkins zenye nguvu ya kilowati 161 kila moja na zinafungwa na mafundi wa Temesa kwa kushirikiana na wale wa kampuni ya Delta Industrial Equipment Limited.
Aliongeza kuwa kazi ya kufunga injini itaenda sambamba na kazi ya kukipaka rangi kivuko hicho na baada ya hapo kivuko kitaendelea kutoa huduma kama hapo awali lakini kwa kasi zaidi na kuongeza kuwa kivuko hicho kina uwezo wa kubeba tani 25 sawa na abiria 100 na magari 3 kwa wakati mmoja.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.