Serikali yapokea maoni kuhusu Tozo za mazao ya Uvuvi Kanda ya Ziwa na kuahidi kuyafanyia kazi.
Serikali imewaomba wafanyabiashara wa mazao ya Uvuvi kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa kuwa na subira na kuendelea kufanya shughuli zao kwa kanuni zilizopo wakati maoni yao kuhusu ongezeko la tozo kutoka Shs 10 hadi 100 likifanyiwa kazi.
Kauli hiyo ya Serikali imetolewa leo kwenye ukumbi mkubwa wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza na Naibu Katibu Mkuu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bi. Agness Meena katika kikao chake na wawakilishi wa wafanyabiashara wa mazao ya uvuvi,amebainisha kuwa maoni yao yatafikishwa kwa mamlaka husika na yatafanyiwa kazi na kutolewa majibu muda mfupi ujao.
Amewaomba wadau hao kuendelea na shughuli zao baada ya kufanya mgomo kwa siku kadhaa kuishinikiza Serikali kubadili tozo hiyo na kubaki ya zanani
"Naomba mtambue mnayo Serikali sikivu kwa wananchi wake ndiyo maana nimefika hapa kuyasikiliza maoni yenu na kwenda kuyafikisha sehemu husika kwa lengo la kuyapatia ufumbuzi,"amesisitiza Mtendaji huyo wa Wizara
Bi.Meena ameongeza kuwa kitendo cha kugoma na shughuli za biashara kusimama siyo njia sahihi bali mazungumzo ya pande zote ndiyo suluhisho.
Awali akimtambulisha Naibu Katibu Mkuu huyo kabla ya kuanza kikao hicho,Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza,Ndg. Elikana Balandya amesema baada ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kuwasikiliza wafanyabiashara hao imefanya jitihada za haraka za kuwasiliana na Wizara husika wakiamini suluhisho litapatikana ili kuwepo na tija kwa upande wa Serikali na wananchi.
"Tumekuwa na wakati mgumu na ongezeko hili kutoka na msururu wa tozo tunazopitia kabla ya mzigo kufika kwa mlaji,tunaomba Serikali mlifanyie kazi suala hili,"Nyahunga Sabaya,mfanyabiashara kutoka Gozba
Tozo hiyo mpya imeanza kutumika rasmi Agosti 5,2023 na kupokelewa kwa mtazamo tofauti hasa kwa wafanyabiashara wa mazao makavu na kusababisha shughuli za biashara soko la Mwaloni Kirumba kusimama kwa siku kadhaa
Kikao hicho kimewasjirikisha wawakilishi wa mazao ya Uvuvi kutoka mikoa ya Mwanza,Kagera,Geita,Mara na Simiyu
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.