Serikali yawahimiza vijana kuchangamkia fursa za mazingira ya kujiajiri wanayoandaliwa.
Serikali imeendelea kuwahimiza vijana kuchangamkia fursa za kujiajiri wakati wakiandaliwa mazingira mazuri ya kumudu hatua hiyo.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe.Abdallah Ulega ametoa kauli hiyo jumanne hii huko Wilayani Misungwi kwenye Shamba
la Taifa la Mifugo wakati wa hafla fupi ya kupokea Lori la Tani 10 na Pikipiki 4 kwa ajili ya mradi wa vijana wanaojihusisha na unenepeshaji mifugo,kiongozi huyo mwandamizi wa Serikali amesema Serikali inatambua mchango wa vijana katika ujenzi wa Taifa hivyo wasikate tamaa.
"Leo napokea msaada huu kwa niaba yenu kutoka marafiki zetu wa maendeleo Shirika lisilo la Kiserikali la Heifer International,hizi ni juhudi zinazofanywa kuhakikisha hampotezi muda wenu hapa badala yake mtoke hapa mkiwa ni wataalam wa uhakika,"Abdallah Ulega,Waziri wa Mifugo na Uvuvi
Mhe. Ulega amebainisha anatambua sekta ya mifugo na Uvuvi ni ya uzalishaji hivyo ni jukumu lao kama Wizara kuendana na maono ya Rais Dkt.Samia kulikomboa kundi kubwa la vijana na kuingia katika hatua ya kujiajiri baada ya kuandaliwa kisasa.
Amewataka vijana hao kutokata tamaa kwani siku zote mambo mazuri hayaji kirahisi ni lazima kupitia changamoto za hapa na pale kufikia mafanikio mazuri.
"Sisi kama Mkoa tumejipanga kuhakikisha malengo yote mazuri kwa vijana yanakuja na matokeo chanya kwa kusimamia na kufuatilia kikamilifu",Emil Kasagara,Katibu Tawala Msaidizi Uchumi na Uzalishaji.
"Tunatambua hatari ya kuliwacha kundi la vijana ambao ni nguvu kazi ya Taifa,sisi kama Heifer International tupo bega kwa bega na Serikali kufikia malengo yaliyo kusudiwa,"Mark Tsoxo,Mkurugenzi mkazi Heifer International.
"Tunaishukuru Serikali ya Rais Samia kwa juhudi za kutuendeleza sisi vijana,mradi huu wa unenepeshaji mifugo utakuwa ni mkombozi kwetu na kuzidi kuiborsha Sekta ya mifugo nchini," Suzana John mnufaika na mradi wa viatamizi.
Jumla ya vijana 900 wapo kwenye Shamba la Taifa la Mifugo wakiendelea kupata mafunzo ya kisasa ya ufugaji wa kisasa ambapo kila mmoja amekabidhiwa ng'ombe 10 kumfuga kisasa na kumuuza na baadaye kujipatia mtaji wa kujiendeleza.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.