Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amezindua Jengo la Wodi ya Saratani katika Hospital ya Rufani ya Bugando ili kupunguza vifo vitokanavyo na saratani kwa kuwa wagonjwa wengi watapata matibabu kwa ukamilifu huku serikali ikitoa kiasi cha shilingi billion 3.1 kwa ajili ya ununuzi wa mashine moja ya mionzi.
Akizindua Jengo hilo Mhe. Dkt Mpango amesema takwimu zinaonyesha ugonjwa wa saratani unaua watu wengi duniani huku nchini kukiwa na ongezeko la ugonjwa huo ambao unawapata watu elfu 42 hasa Kanda ya Ziwa ambapo Serikali imetoa millioni 500 kwa ajili ya kusaidia utafiti wa ugonjwa huo unaofanywa na madaktari bingwa wanaotoka katika hospital hiyo.
Amesema Serikali inaendesha harakati za kupambana na ugonjwa huo huku elimu za kuondokana na viatarishi vinavyochangia kuondokana na hatari hizo zikiwemo ufanyaji mazoezi ,umuhimu wa chakula,kupunguza matumizi ya pombe kutasaidia kukabiliana tatizo hilo.
Awali akiwasilisha taarifa ya mradi wa Ujenzi wa Jengo la Wodi ya Saratani Mkurugenzi Mtendaji wa hospital hiyo Dkt.Fabian Massaga amesema tatizo la saratani bado ni kubwa Kanda ya Ziwa watu elfu 45 wanaugua saratani hivyo iliwalazimu kuchukua sampuli za damu katika mikoa nane ya Kanda ya Ziwa kwa ajili ya kufanya utafiti wa chanzo cha ugonjwa huo.
Ameongeza kuwa, mradi huu ulianza Septemba 1 mwaka 2020, kwa sasa umefikia asilimia 96, kazi zilizobaki ni za umaliziaji, ambazo zitakamilika hivi karibuni pia jengo hilo lenye ghorofa tatu lina ukubwa wa mita za mraba 4,100.
Aidha, matibabu ya Saratani katika hospitali hiyo yalianza Mwaka 2009 ambapo dawa za kemikali (chemotherapy) zilikuwa zinatolewa , kutokana na ongezeko kubwa la wagonjwa wa Saratani, hospitali ya Bugando kwa kushirikiana na Serikali na Shirika la Kimataifa la Nguvu za Kiatomiki (International Atomic Energy Agency) waliandaa mpango wa kupanua huduma za matibabu ya Saratani katika hospitali hiyo.
Vilevile mpango huu ulikuwa wa awamu mbili awamu ya kwanza ilihusisha ujenzi wa jengo maalumu la kusimika mashine za matibabu ya mionzi ambalo lilikamilika mwaka 2015 na kuanza kutumika mwaka 2017 baada ya ununuzi na usimikaji wa mashine za matibabu ya saratani kwa njia ya mionzi huku awamu ya pili ilihusisha ujenzi wa jengo la kulaza wagonjwa wa saratani (oncology ward).
"Hospitali ya Bugando ni hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Ziwa, kanda ambayo ina watu zaidi ya Milioni 17 katika Mikoa yote 8 inahudumia mikoa yote na baadhi ya Mikoa ya Kanda ya Kati na Nyanda za Juu Kusini jengo hili lina umuhimu kwa sababu idadi ya wagonjwa wa Saratani watakaopata matibabu hapa itaongezeka"alisema Dkt.Massaga.
Amesitiza kuwa Huduma zinazotolewa kwenye jengo hili ni matibabu kwa njia ya mionzi na dawa za kinyuklia huduma hizo zitatolewa kwenye sakafu ya ardhini, huduma ya kuona wagonjwa wa nje na matibabu ya utoaji wa dawa kwenye sakafu ya kwanza, pamoja na huduma ya kulaza wagonjwa wodini kwenye sakafu ya pili na ya tatu, ambapo jengo hilo linakusudiwa kua na vitanda vya wagonjwa 120, pamoja na huduma zingine zinazo husiana na matibabu ya ugonjwa wa saratani.
Aliongeza kuwa, Mradi huu hadi kukamilika kwake unabajeti ya kiasi cha Sh. bilioni 5.4, hadi sasa mradi huu umesha tumia takribani kiasi cha Sh bilioni 4.7 katika kununua vifaa vya ujenzi, kumlipa mkandarasi mjenzi na Mhandisi mshauri.
Hata hivyo, ili huduma zilizo kusudiwa ziweze kutolewa kwa ufanisi kama zilivyo kusudiwa upo uhitaji wa vifaa vya ujenzi, miundombinu ya kuzuia mionzi, samani za kutumika kwenye jengo hili na vifaa tiba kwa ujumla wa mahitaji hayo ni takribani Sh. bilioni 12 ambayo yameshawasilishwa Wizara ya Afya.
"Matarajio yetu mradi utakapokamilika utakuwa na faida nyingi ikiwemo kuongezeka kwa ubora wa huduma kwa wagonjwa wa saratani wanaopata matibabu hapa kwakuwa watakuwa na sehemu nzuri na ya kisasa ya kupumzika wakati wanapata matibabu,kupungua kwa gharama za malazi hasa kwa wagonjwa wanaotoka mikoa ya mbali waliolazimika kupanga kwenye mahoteli nje ya hospitali wakati wa kupata matibabu." Alieleza Dkt. Massaga.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe.Adam Malima ameishukuru sana serikali ya awamu ya sita inayoogozwa na Mhe.Samia Suluhu Hassan kwa kudumisha ushirikiano na wadau huduma hii inamafanikio makubwa kwa wananchi kwa sababu zinapunguza uzito wa wananchi kwenda mbali kutafuta matibabu kuwepo kwa huduma hii ni mkombozi kwa kwa wananchi.
Aliongeza kuwa matarajio ya Mkoa wa Mwanza ni kuwa kitovu cha huduma za afya Kanda ya Ziwa na Magharibi pia tutadumisha uhusiano na wadau na taasisi za afya ili kuwepo kwa huduma bora na zenye tija kwa jamii.
Kwa upande wake, Mhashamu baba Askofu wa Jimbo la Kigoma na Mwakilishi wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania Mhe. Joseph Mlola akitoa neno wakati wa Misa ya Uzinduzi wa Jengo hilo amesema wagonjwa watakaokuja kutibiwa katika Jengo la Saratani wapate uponyaji wa haraka na amewashukuru wote waliofanikisha ujenzi wa jengo hilo hadi kukamilika kwani limeleta amani,furaha na faraja kwa wagonjwa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.