Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Bw. Balandya Elikana ameupongeza na kuushukuru uongozi wa benki ya stanbic kwa kuchangia vifaa tiba vyenye thamani ya zaidi ya shilingi Milioni 19 ambavyo vitaenda kuwa na mchango mkubwa katika hospitali na kuboresha huduma za afya.

Amesema hayo leo Novemba 27, 2025 wakati akimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mwanza katika hafla ya kukabidhiana vifaa tiba ambavyo ni viti mwendo 10, vitanda na magodoro yake 10 pamoja na mashuka 200 kwa hospitali za Wilaya za Nyamagana na Ilemela iliyoandaliwa na benki ya Stanbic katika viwanja vya ofisi ya Mkuu wa Mkoa.

Bw. Balandya amesema kuwa serikali imeendelea kufanya jitihada za kupambana na adui wa maendeleo ambae ni maradhi na kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya na kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika shudhuli za ujenzi wa taifa kwakua sekta ya afya ni sekta muhimu sana kwa maendeleo ya wananchi.

“Sekta ya afya ni sekta muhimu sana kwa maendeleo ya wananchi popote pale duniani na kwa kutambua hili hata Baba wa Taifa letu Mwalimu Julius Nyerere wakati akitaja maadui wa taifa letu alijumuisha suala la afya”. Amesema Bw. Balandya.

Sambamba na hayo amewasihi wananchi kuendelea kujitokeza hospitali na vituo vya kutolea huduma za afya kwa wakati ili waweze kujua hali ya miili yao kwa kupima na kupata huduma za matibabu kwa wakati.

Naye Meneja wa benki Stanbic tawi la Mwanza Bw. Geoffrey Makondo amesema utoaji wa huduma bora kwa jamii ni kwa kuanza kutoa misaada kwa jamii husika na wao wamechagua kuigusa jamii ambayo wanafanya nayo kazi kila siku kwa kuichangia katika sekta ya afya.

Ameongeza kuwa katika kutimiza miaka 30 ya kihudumia jamii benki itaendelea kushirikiana vyema na serikali pamoja na watumishi wake ili kuhakikisha wanaendelea kukuza shughuli za kiuchumi na maendeleo katika taifa.

Akimuwakilisha Mganga Mkuu Mkoa wa Mwanza, Dkt. Kwandu Mashuda ameishukuru benki ya Stanbic kwa kuikumbuka idara ya afya kwakua ni idara nyeti na yenye uhitaji mkubwa na amesema wataenda kuvitumia vyema vifaa hivo na kuleta tija kwa wagonjwa.

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.