Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), Japhet Justin amesema hadi kufikia Februari mwaka huu benki hiyo imefikia mtaji wa Sh.bilioni 68.
Ametoa kauli hiyo leo Machi 19, 2019 katika uzinduzi rasmi wa benki hiyo katika kongani ya kanda ya ziwa unaofanywa na Waziri Mkuu Mhe.Kassimu Majaliwa jijini Mwanza.
Justin amesema kiasi hicho ni sawa na ongezeko la asilimia 13 ya Sh.60 bilioni walizopewa na Serikali mwaka 2015 ilipoanza kufanya kazi rasmi.
"Mpaka sasa tumeshatoa mikopo yenye thamani ya Sh.107 bilioni na kati ya fedha hiyo tayari imesharejeshwa Sh.31.4 bilioni ," amesema Justin.
Ameongeza kuwa katika upande wa kilimo cha pamba kwa mwaka 2018 benki hiyo ilitumia Sh.6.6 bilioni kwa ajili ya kununua pembejeo na viuatilifu kwa wakulima zaidi ya laki 2.
"Upande wa Kahawa tulitumia Sh.30 bilioni na kwa sasa kuna ekari zaidi ya 2000 wilayani Buchosa ambazo zimetengewa zaidi ya Sh. Bilioni 2.
Kuhusu alizeti amesema wametenga Sh. Milioni 800 kujenga kiwanda cha Alizeti wilaya ya Kahama Mkoani Shinyanga na katika ufugaji, benki inatarajia kufungua kiwanda ambacho kitakuwa na uwezo wa kuchinja ng'ombe 125 ambapo wametenga Sh.bilioni 8 kwa ajili ya kiwanda hicho.
Ameongeza kuwa katika sekta ya uvuvi pia wametenga Sh.bilioni 40 ambazo zitakopeshwa katika sekta hiyo ili kujenga viwanda vya kuchakata samaki.
Aidha, Mwenyekiti wa bodi ya Wakurugenzi wa benki hiyo Rosebert Kulwijila amesema tangu benki hiyo ianzishwe wameshakopesha matrekata 50 kwa wakulima katika mikoa ya kanda ya ziwa.
Amesema jumla ya wakulima 6,864 watanufaika na matreka hayo yanayoendelea kutolewa na benki hiyo ambapo kwa leo pia waziri mkuu atakabidhi matreka 16 kwa viongozi wa vyama vya ushirika
Naye Mkuu wa mkoa wa Mwanza Mhe.John Mongella amesema Mkoa una benki 28 za kibiashara zenye matawi 26 kwenye halamshauri zote za mkoa huo sawa na zaidi ya asilimi 90 ya benki zote.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.