Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa kushirikiana na idara na sekta mbalimbali ambazo ziko chini ya wizara hiyo wameadhimisha wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani iliyofanyika Kitaifa Mkoani Mwanza kwa kutoa huduma tofautitofauti kwa wananchi ikiwemo kufanya vipimo vya magonjwa mbalimbali, kukusanya damu, chanjo ya Uviko 19 na kutoa elimu jinsi ya kujikinga na ajali.
Maadhimisho ya wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani yalifanyika Mkoani Mwanza katika Uwanja wa Furahisha uliopo Wilaya ya Ilemela kuanzia Machi 14 hadi 17, 2023 yakiwa na Kauli Mbiu isemayo Tanzania bila ajali inawezekana-Timiza wajibu wako.
Idara na Sekta zilizoshiriki kutoa huduma hizo ni Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza Sekoutoure, Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Ziwa Bugando(BMC), Hospitali ya CF, Msalaba Mwekundu(RED CROSS) Shirika la Kuhudumia Watoto Duniani (UNICEF) na Ofisi ya Kanda ya Ziwa ya Damu Salama.
Akizungumzia huduma hizo, Mratibu wa Huduma za Maabara na Damu Salama Mkoa wa Mwanza, Juma Shigella, alisema Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Ziwa Bugando(BMC) na Hospitali ya CF zilifanya vipimo vya magonjwa mbalimbali kwa wananchi, RED CROSS) ilitoa elimu kwa wananchi jinsi ya kujikinga na ajali, UNICEF iliratibu utoaji wa chanjo ya Uviko 19 na Ofisi ya Kanda ya Ziwa ya Damu Salama kwa kushirikiana na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza Sekoutoure walifanikiwa kukusanya jumla ya chupa 35 za damu.
“Tuliona tutumie Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani kwa ajili ya kukusanya damu kwa hiari kutoka kwa wananchi ambao wanatembelea mabanda yetu ingawa maadhimishio haya yanaenda sambamba na utoaji wa elimu lakini huduma ya damu salama ni muhimu sana kwa sababu ajali nyingi zinapotokea watu wengi wanapoteza damu hivyo ili kuokoa maisha yao huhitaji damu, tuliona kuna umuhimu wa kukusanya damu katika mkusanyiko huo,”alisema Shigella na kuongeza
“Tunaishukuru sana Wizara ya Ofisi ya Rais TAMISEMI kama viongozi wetu ambao ndiyo dira yetu katika utoaji wa huduma za afya wamekuwa nasi katika kipindi cha wiki nzima ya maadhimisha haya tumetoa huduma za upimaji wa magonjwa mbalimbali kwa wananchi ikiwemo Virusi vya Ukimwa(VVU) na kisukari.
“Pia tumetoa elimu kuhusiana na lishe bora kwa kuzingatia makundi ambayo yanahitajika mwilini ili kupunguza vyakula ambavyo havihitajiki kwa ajili ya afya, namna ya kujikinga na ajali, namna ya kujikinga na magonjwa mbalimbali na upimaji wa macho,”alisema Shigella.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.