Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini TASAF III Wilayani Ilemela Mkoani Mwanza inatekeleza Ujenzi wa Zahanati pamoja na Nyumba ya Mtumishi kwenye Mtaa wa Mihama katika kata ya Kitangiri kwa zaidi ya Tshs. Milioni 219.
Akizungumza na wananchi wa Mtaa wa Mihama na Jiwe kuu alipofanya ziara ya kukagua ujenzi huo Mhe. Jenista Mhagama Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejomenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora amemshukuru Rais Samia kwa miradi hiyo na Viongozi wa Mkoa kwa Usimamizi pamoja na wananchi kwa uzalendo na kujituma kwa kuchangia kuchimba msingi, kusogeza mawe na kusomba mchanga.
"Mifumo imefunguka, fedha zipo na wananchi wapo hivyo hatuna haja ya kuchelewesha miradi mikubwa ya namna hii, tuna kila sababu ya kuhakikisha miradi hii inakamilika kwa masilahi ya wananchi akina mama na watoto watakaonufaika sana na huduma za afya na mkikamilisha kwa wakati tunaleta miradi mingine kumi kwa wananchii" Mhe. Mhagama.
Aidha, amewaagiza viongozi wa Wilaya hiyo kukamilisha taratibu za kupata vikundi vya uchumi chini ya mradi wa TASAF vyenye sifa ili waweze kujikwamua kwa kuwaletea vikundi vingine na ametaka taratibu za kisheria zifuatwe katika kuwapata wanufaika wa miradi ya uhaulishwaji wa fedha ili pasiwe na upendeleo bali wapate wenye sifa.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Adam Malima amemhakikishia Waziri Mhagama kukamilisha Ujenzi wa Zahanati na Nyumba ya mtumishi kwenye mtaa wa Mihama ili wananchi waanze kupata huduma za afya kufikia Machi 28, 2023 hasa kwa huduma za afya ya Mama na Mtoto na Lishe.
Vilevile, Mhe. Hassan Masala, Mkuu wa Wilaya ya Ilemela ametumia wasaa huo kumshukuru Mhe. Rais kwa kuwaletea Miradi ya TASAF wananchi wa Kata ya Kitangiri huku akibainisha kuwa imeendelea kuleta chachu kwenye maendeleo na amewapongeza wanannchi wa kata hiyo hasa wa Mitaa ya Jiwe Kuu na Mihama kwani awali wananchi walikua na kiu ya kupata zahanati kwenye eneo lao.
"Miradi hii ikikamilika itatumia kiasi cha TSh. 219,259,541.55 ambapo fedha toka TASAF III ufadhili wa TPRP IV – OPEC IV ni Shilingi 187,366,541.55 sawa na asilimia 85% wakati michango ya wananchi ina thamani ya Shilingi 31,893,000 sawa na 15%." Amesema Leonard Robart, Mratibu wa TASAF Wilaya ya Ilemela.
"Tasaf wametuwekea historia kwenye kata yetu, wamesababisha tuanze maendeleo ya kasi sana kwenye sekta ya afya maana mwezi wa nne tutaanza kupata huduma za Afya kwenye kata yetu na kwakweli nawapongeza na kuwashukuru sana wananchi wanaojitolea nguvu zao kuhakikisha zahanati hii inajengwa" Mhe. Donald Protas Diwani wa Kata ya Kitangiri.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.