Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imesema kuanzia Januari Mosi, 2020 kila mtu atatakiwa kumiliki laini moja ya kampuni moja ya simu ya mkononi.
Kauli hiyo imetolewa na Meneja wa TCRA kanda ya Ziwa, Mhandisi Francis Mihayo katika mkutano wa wadau wa sekta ya mawasiliano uliolenga kupokea kero na mapendekezo juu ya utendaji wa mamlaka hiyo.
Mkutano huo ulishirikisha viongozi wa dini mbalimbali,wamiliki wa vituo vya redio, mitandao ya kijami na mafundi simu ambapo wengi wao waliomba TCRA kushirikiana na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) ili kuweza kupata vitambulisho kwa wakati.
Mhandisi Mihayo alisema kwa mtu atakaye hitaji kuwa na laini mbili atatakiwa kuandika maelezo ya uhitaji huo.
Alisema, imelazimika kuunda kundi maalum ‘group’ linaloshirikisha watoa huduma za mawasiliano nchini kwa ajili ya kuziharibu simu za matapeli wanaotuma ujumbe mfupi wa maneno (sms) kwa watu ili kujipatia fedha kwa njia zisizo rasmi.
Pia imewaonya watu maarufu wakiwamo wanasiasa wanatumia mitandao ya kijamii kusambaza taarifa ambazo zinapotosha jamii kuhusu jambo lolote na kuwataka kuacha mamlaka husika au vyombo vya habari kusema kwa kuzingatia maadili ya kazi zao.
“Moja ya malalamiko sugu katika suala la mawasiliano ni watu kutumia ujumbe wa utepeli, kweli watu wametapeliwa sana, wapo wanaolalamika kupata ujumbe usiku na kusababisha mgogoro katika ndoa lakini kama TCRA na watoa huduma tukaamua kuunda group letu la kuwashughulikia watu wa namna hiyo”alisema
Mhandisi Mihayo alisema TCRA imeendelea kutoa elimu kwa jamii ikiwa ni pamoja na kufanya mikutano, kuchapisha majarida, vyombo vya habari lengo likiwa ni kujua namna ya kutumia sekta ya mawasiliano kwa faida na kuziomba taasisi za dini kuelimisha waumini wao.
Alisema mmomonyoko wa maadili katika familia umetokana na wazazi kuwaruhusu watoto wadogo kutumia simu za mikononi jambo ambalo linawafanya kuangalia picha za ajabu.
Mhandisi Mihayo alisema, baadhi ya watu maarufu wamekuwa wakitumia mitandao ya kijamii kuandika mambo yasiyo ya kweli huku jamii ikiwaamini kuliko vyombo vya habari vyenye leseni na kuwataka kuwa makini na taarifa wanazoweka mitandaoni kwani wanawafuatilia kwa ukaribu.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.