**TEMESA watakiwa kuboresha huduma ili kujenga imani kwa wateja wao*
Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) wametakiwa kubadilika na kuboresha huduma zao kwa wateja ili kuwa mfano wa utoaji wa huduma bora.
Akifungua Warsha ya Wadau wa TEMESA leo kwa niaba ya Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza, Katibu Tawala Msaidizi Mipango na Uratibu Ndg.Joachim Otaru amesema kwa muda mrefu Taasisi hiyo imekuwa ikilalamikiwa kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo huduma duni, kutokuwa waaminifu wa vipuri,na ucheleweshaji wa matengenezo ya magari.
Otaru amebainisha baada ya Serikali ya awamu ya Sita kuanza kuiboresha Taasisi hiyo kuanzia ngazi ya uongozi, fedha na vifaa,sasa ni jukumu la TEMESA kutoa huduma zenye tija.
" Kabla sijaingia kufungua Warsha hii nimeoneshwa hapo aina ya huduma mnazotoa kwenye magari na mitambo mkiwa na vifaa vya kisasa pamoja na gari maalum la utoaji wa huduma na nimeambiwa vifaa hivyo vipo nchi nzima,hongereni sasa onesheni ubora wenu," amesema Otaru.
Ameongeza kuwa wateja wote wanaodaiwa na TEMESA wafanye hima kulipa madeni yote ambapo Mkoa wa Mwanza una wadai wateja wake deni la zaidi ya Shs Bilioni 1.45,fedha ambazo ni nyingi zinazochongia kurudisha nyuma utoaji wa huduma.
"Tumezifanyia kazi changomoto nyingi zilizokuwa zinatukabili ambapo Mafundi wetu wanaendelea kupatiwa mafunzo kwenye vyuo mbalimbali,Karakana zetu zote 13 nchini tumefunga camera za kisasa za kubaini aina yoyote ya wizi wa vipuri,kwa kifupi utoaji wa huduma zetu umekuwa wa kiwango kizuri tofauti na hapo awali," Mhandisi Hussein Karonda,Kaimu Mtendaji Mkuu,TEMESA.
"Kituo chetu cha Mwanza licha ya kuwadai wateja wetu fedha nyingi lakini tunashukuru Serikali imezidi kutuwezesha kila mwaka,mfano mzuri ni vifaa hivi na gari maalum lenye gharama ya Shs Milioni 700 vinavyotupa ari ya utoaji wa huduma bora kwa magari na mitambo ya Serikali," Mhandisi Gilly Gabriel Chacha,Meneja wa TEMESA Mwanza.
Aidha baadhi ya Wadau wa Taasisi hiyo wamepatiwa hati maalum kutokana na kutambua mchango wao akiwemo aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe.Adam Malima na baadhi ya Wazabuni wa Vipuri wanaoendelea kushirikiana na TEMESA kutoa huduma kwa wateja.
Warsha hiyo yenye lengo la kuwasikiliza Wadau kuhusiana na changamoto zilizopo na kuzipatia ufumbuzi imewashirikisha Makatibu Tawala wa Wilaya zote za Mwanza,Mameneja wa Mikoa wa TEMESA,Wakurugenzi wa Halmashauri za Mwanza pamoja na Wazabuni wa Vipuri.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.