Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) imeushauri Wakala wa Vivuko na Umeme (TEMESA) kuongeza ukusanyaji wa mapato na kuimarisha udhibiti wa mianya ya upotevu mapato iweze kujiendesha badala ya kutegemea ruzuku ya serikali.
Pia TEMESA kwa kushirikiana na uongozi wa TASAC na vyombo vya usalama waunde kamati itakayoshughulikia utatuzi wa changamoto ya shughuli za uvuvi zinazofanyika kwenye njia za vivuko na kuielimisha jamii madhara yanayoweza kuathiri vyombo vya usafiri wa majini.
Agizo hilo limetolewa na Mwenyekiti wa Bodi ya TASAC, Profesa Thadeo Satta kwa niaba ya wajumbe wa bodi hiyo baada ya kutembelea na kukagua vivuko vya MV. Mwanza na MV. Misungwi vinavyotoa huduma ya usafirishaji wa abiria na mizigo kati ya Kigongo, wilayani Misungwi na Busisi, Sengerema.
Alisema ili wakala huo ujiendeshe wenyewe, uongeze juhudi kwenye ukusanyaji wa mapato na kudhibiti mianya ya upotevu ili fedha za ruzuku zinazotolewa na serikali zikahudumie sekta zingine.
Mwenyekiti huyo wa bodi ya TASAC alisema, vivuko vya TEMESA vinatoa huduma kwa wananchi na havifanyi biashara ili kupata faida ambapo serikali imekuwa ikitoa ruzuku inayotumika kujenga vivuko vipya na ukarabati wa vivuko vyenye hitlafu na uchakavu wa mitambo, hivyo TASAC imeridhishwa na bajeti ya wakala huo wa vivuko na ufundi wa umeme.
“TASAC ipo kwa ajili ya kuangalia masuala ya kiusalama na hapa kaimu meneja wa TEMESA ameeleza changamoto ya shughuli za uvuvi zinazofanyika kwenye njia za vivuko zinaathiri na zinahatarisha usalama wa abiria na vivuko vyenyewe.Tunaelekeza waunde kamati ya utatuzi wa tatizo hilo kwa kuwaelimisha wavuvi na jamii ili kulinda usalama wa abiria na vyombo vyenyewe,”alisema Profesa Satta.
Alisema serikali imeweka vyombo hivyo kuwahudumia wananchi kutoka upande mmoja kwenda ng’ambo ya pili na ili kunusuru maisha ya watumiaji wa vivuko wavuvi waache kufanya shughuli zao kwenye njia za vivukokwani wanaisababishia serikali hasara.
Awali Kaimu Meneja wa TEMESA Mkoa wa Mwanza Abdallah Atiki, alisema wakala huo unajiendesha kwa kutumia mapato ya ndani na mwaka huu imetenga bilioni 16 kwa jili ya kuhudumia vivuko vyote nchini na wameimarisha usalama na mifumo wa ukusanyaji wa maduhuri ya serikali.
Alisema mwaka 2018/2019 kwa kutumia vikosi vyake vya ufundi,walifanya matengenezo kinga kwa vivuko na kuondoa vipuri chakavu na kuviwezesha kuwa salama, kutoa huduma bora za uhakika kwa saa 24 na usalama wa abiria na mizigo.
Atiki alisema wanakabiliwa na changamoto ya watu binafsi kusafirisha abiria kwa kutumia mitumbwi na injini isiyo salama katika baadhi ya maeneo yanayohudumiwa na vivuko vya TEMESA, wavuvi kuendesha shughuli zao (kutega nyavu) kwenye njia za vivuko.
“Tuna changamoto ya vyombo binafsi visivyo salama kusafirisha abiria kwenye maeneo yenye vivuko mbali na kuhatarisha usalama wa abiria vinachangia kupunguza mapato.Pia zana za uvuvi kutengwa kwenye njia za vivuko zikinasa kwenye mifumo ya injini zinahatarisha usalama na uharibifu wa chombo,” alisema.
Kwa mujibu wa meneja huyo hadi mwaka 2018/2019 walikusanya maduhuri ya serikali sh. bilioni 5.7 ambapo makadirio ya bajeti ya mwaka 2019/2020 ni kukusanya sh. bilioni 7 lakini kwa hali ilivyo wanaweza kukusanya bilioni 6 chini ya lengo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.