Imeelezwa kuwa afya ya watumiaji bidhaa mbalimbali zitalindwa na kuboreshwa ikiwa sheria ya Chakula, Dawa na Vipodozi sura 219, itasimamiwa na kutekelezwa ipasavyo huku vyombo vya habari vikitimiza wajibu wao kwa usahihi.
Hayo yalisemwa na Mkurugenzi Msaidizi wa Habari Maelezo Zamaradi Kawawa katika kikao kazi cha Wahariri na Waandishi wa Habari kutoka mikoa ya Mwanza na Shinyanga kuhusu uhamasishaji wa sheria ya Chakula,Dawa na Vipodozi sura 219 kilichoandaliwa na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) kilichofanyika mkoani hapa.
Kawawa alisema, wahariri na waandishi wa habari wanamchango mkubwa katika kuhimiza utekelezaji wa sheria hiyo,kuelimisha umma kwa kuwapatia taarifa sahihi zinazohusu shughuli za udhibiti wa bidhaa hizo kutoka vyanzo mbalimbali sambamba na kuijua sheria hiyo.
Alisema, vyombo hivyo vinawajibu wa kutumia kalamu zao kuleta mabadiliko chanya katika jamii kuhusu udhibiti wa bidhaa,kuielimisha juu ya kuzingatia ubora na usalama wa bidhaa hizo pamoja na kuwaibua watu wanaovunja sheria hiyo kwa kutoa taarifa TFDA na kwa vyombo vingine vya sheria vinavyohusika na udhibiti.
“Wana habari waendelee kutoa elimu kwa jamii juu ya madhara watakayo yapata kiafya endapo watatumia bidhaa za chakula,dawa,vipodozi,vifaa tiba na vitendanishi ambayo vipo kinyume na sheria sambamba na kutoa mapendekezo kwa TFDA juu ya namna ya kuboresha usimamizi na utekelezaji wa sheria,”alisema Zamaradi.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu TFDA Agnes Kijo alisema,suala la afya ni la jamii nzima,hivyo ni wajibu wakila mtu katika kudhibiti bidhaa bandia na duni,huku waandishi wakiendeleza ushirikiano na mamlaka hiyo katika kuibua wafanyabiashara ambao siyo waaminifu wanaouza bidhaa zilizopita muda.
Kijo alisema, kwa mwaka wanatumia zaidi ya milioni 100 katika kufanya opareshini na ukaguzi maalum wa kudhibiti bidhaa hizo,hivyo ni vyema wananchi wakahamasishwa na kuelimishwa kuacha kutumia ili fedha hizo zitumike kwenye miradi ya maendeleo.
Naye Mwanasheria Mshauri wa TFDA Iskari Fute alisema,madhumuni ya sheria ni kuweka mfumo thabiti wa usalama,ubora na ufanisi wa chakula,dawa,vipodozi,vifaa tiba, vitendanishi,vifaa vya maabara na dawa zenye asili ya miti shamba pamoja na kulinda afya ya jamii ili kutekeleza msingi wa haki ya kuishi.
Hata hivyo Mkurugenzi wa Dawa na Bidhaa Nyongeza wa TFDA Adam Fimbo alisema, bidhaa wanazodhibiti ni zile zenye athari moja kwa moja katika afya ya binadamu,hivyo waandishi wa habari wanamchango mkubwa wa kuelimisha jamii kuhusu matumizi sahihi ya bidhaa hizo.
Aidhaa baadhi ya washiriki wa kikao hicho,waliitaka mamlaka hiyo kufika hadi maeneo ya vijijini kutoa elimu kuhusu madhara yatokanayo na utumiaji wa vipodozi vyenye viambato vyenye sumu na bidhaa bandia na duni.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.