TIMIZENI NDOTO ZA RAIS SAMIA KUWALETEA MAENDELEO WANANCHI : KATIBU MKUU TAMISEMI
Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza Balandya Elikana leo Aprili 5,2024 amefungua rasmi Mkutano Mkuu wa Jumuiya ya Serikali za Mitaa Kanda ya ziwa (LVRLAC) na kutoa rai kwa wajumbe kuhakikisha wanatimiza ndoto za Rais Samia za kuwaletea maendeleo wananchi kutokana na miradi iliyoelekezwa kwenye Halmashauri zao.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu (OR-TAMISEMI) Balandya amesema Serikali ya awamu ya sita imeleta miradi mingi hasa mkoa wa Mwanza hivyo ni wajibu kwa wakurugenzi, Meya na Madiwani kuhakikisha miradi hiyo inasimamiwa kikamilifu ili iwe na tija kwa wananchi.
"Ndugu wajumbe wa LAVRLAC Tanzania tuna bahati ya ziwa Victoria sehemu kubwa kuwa huku kwetu,fursa za uchumi wa bluu umezidi kuongezewa nguvu kwa Serikali kuiboresha sekta ya uvuvi kwa ufugaji wa samaki kutumia vizimba,juhudi hizi ni lazima zilete matokeo chanya kwa usimamizi mzuri kwetu sisi tuliopewa dhamana ya uongozi",amesisitiza mtendaji huyo wa mkoa.
Balandya ameipongeza Jumuiya hiyo kwa juhudi zake za kuziwezesha Halmashauri miradi iliyofikia thamani ya zaidi ya shs bilioni 20 huku ikiendelea na mikakati ya utunzaji mazingira na mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi.
"Hizi safari zenu za mara kwa mara nje ya Tanzania niwasihi mzitumie vizuri kujifunza kutoka kwa webzetu waliopiga hatimua katika utaalamu hasa mabadiliko ya tabia nchi,wananchi wetu wanajikuta wanaharibikiwa na mazao au kutokea kwa ukame,"amesisitiza Balandya.
Mtendaji Mkuu wa LAVRLAC Bill Brown amesema mkutano huo mkuu wajumbe watapata nafasi ya kujadiliana changamoto zilizopo na kuweka mikakati ya kumletea maendeleo mwananchi.
"Wizara hii ya Tamisemi inatengewa fedha nyingi kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo,hivyo nyie Wakurugenzi na Madiwani tunawahimiza mkasimamie kwa umakini na uadilifu mipango hii ya kuwaletea maendeleo wananchi,"Steven Matambi,Kaimu mkurugenzi wa Serikali za mitaa,Tamisemi.
Washiriki wa mkutano huo ni wakurugenzi wa Halmashauri,Madiwani,Wenyeviti wa Halmashauri wanatokea mikoa ya Mwanza,Kagera,Simiyu,Mara,Geita na Shinyanga.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.