TUME HURU YA UCHAGUZI YATAKA SHERIA NA TARATIBU ZA UBORESHAJI DAFTARI ZIZINGATIWE
Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Magdalena Rwebangira amewaasa Maafisa Uandikishaji Mkoani Mwanza kwenda kutoa mafunzo ya nadharia na vitendo katika ngazi za kata kwa kuzingatia, sheria, taratibu na kanuni za tume hiyo.
Ametoa wito huo leo Agosti 11, 2024 wakati akihitimisha mafunzo ya siku mbili ya watendaji wa ngazi ya Mkoa kuhusu uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura yaliyofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza huku yakiwakutanisha wajumbe wa majimbo yote ya Mkoa huo.
Mhe. Rwebangira amewataka maafisa hao kuwasiliana na tume mara kwa mara endapo litatokea jambo la kuhitaji ufafanuzi ili kuhakikisha wanatekeleza kwa ukamilifu majukumu waliyopewa kwa maslahi ya zoezi hilo.
Aidha, amewataka watendaji hao kuwa makini kwenye usambazaji na utunzaji wa vifaa, matumizi ya lugha nzuri na kusimamia waandikishaji ili wafanye kazi muda wote kwenye vituo vya kuandikishia hata kama hakutakua na wahitaji.
Naye mshiriki Emanuel Sherembi ambaye ni Mwenyekiti wa mafunzo hayo amefafanua kuwa kwa siku mbili hizo wamepata mafunzo ya nadharia na vitendo juu ya ujazaji wa fomu mbalimbali, namna ya kuandikisha wapiga kura, mfumo wa uandikishaji, mapokezi ya vifaa na usimamizi wa fedha.
"Washiriki wote wameelewa na wamefanya mazoezi kwa vitendo na kwa uwezo waliojengewa utawafanya kwenda kufanya kazi hiyo nyeti kwa weledi mkubwa na Mwanza itafanikisha vema zoezi hilo." Amejinasibu mwenyekiti Sherembi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.