Tumieni fursa za Ufugaji na Kilimo kujihakikishia vipato vyenu baada ya kustaafu: RAS Balandya
Umoja wa wazee Mkoani Mwanza, UWAMKOMWA umekumbushwa kuutumia umoja huo katika kuelimishana kuhusu fursa zilizopo hivi sasa katika sekta ya kilimo na ufugaji ambazo zitakuwa mkombozi wa vipato vyao baada kustaafu.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza Ndg. Balandya Elikana ametoa rai hiyo leo wakati wa mkutano na umoja wa wazee hao uliofanyika kwenye ukumbi wa jengo la Nyanza kwa lengo la kujitambulisha rasmi, Balandya amelitumia jukwaa hilo kuwafahamisha wapo baadhi ya wazee baada ya kustaafu wanapata shaka na hatma ya maisha yao wakati zipo fursa za kuendesha maisha yao bila kutumia nguvu nyingi kama alivyokuwa kazini.
"Ndugu Mwenyekiti wa umoja huu mzee wangu Masalakulangwa hapa nimekuja na timu ya wataalamu wa kilimo na mifugo kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa ambao watawasaidia kuwaelimisha na kuwafafanulia masuala mbalimbali ambayo yalikuwa ni changamoto kwenu,Serikali imetenga fedha nyingi kwa lengo la sekta hiyo sasa iwe na tija na siyo kama zamani kutumia uzoefu tu,"amefafanua Mtendaji huyo wa Mkoa.
Balandya amebainisha sasa hivi kwenye shamba la mifugo Mabuki kuna elimu inaendelea kutolewa namna ya ufugaji wa Ng'ombe kitaalamu kwa muda mfupi ambaye anakuja kutoa lita nyingi za maziwa na mwenye uzito wa kutosha wa kulimudu soko la nyama.
"Nawasihi sana wazee wangu tufike hapo Mabuki ili mfaidike na mageuzi haya kwenye kilimo na kuondokana na ufugaji wa ng'ombe wengi wasio na tija,"Balandya.
Mwenyekiti wa umoja wa wazee Mwanza,Charles Masalakulangwa amesema lengo la umoja huo ni kuwa na Wazee wenye busara na maadili mema watakao weza kuishauri vizuri Serikali masuala mbalimbali.
"Tuchangamkie pia Zabuni za kufanya usafi zinazotolewa na Halmashauri zetu,undeni vikundi msajili ili mjihamikishie hizo kazi ambazo zitawafanya msiwe watu wa kukaa na kusubiri siku za malipo ya Pensheni na badala yake zitawaimarishia pia afya zenu kwa kujishughulisha,"Janeth Shishila,Afisa Maendeleo ya Jamii
"Sasa hivi upo ufugaji wa kisasa wa samaki kwenye vizimba mnaweza kuunda umoja wenu au mtu mmoja mmoja na kujikuta mnapata faida kwa muda mfupi,nawakaribisha pia kwenye maonesho ya Nananane mje kupata ufahamu wa fursa mbalimbali zitakazo kuwa na faida kwenu,"Emil Kasagara,Katibu Tawala Msaidizi,Uchumi na Uzalishaji.
"Mnada wa mifugo wa Nyamatala uliopo Wilayani Misungwi haujafungwa kama inavyodhaniwa bali shughuli zake zimepungua siyo kama zamani kutokana na wafugaji wengi kuleta mifugo yao nje ya muda,lakini bado ni mnada muhimu na Serikali inaendelea kutoza ushuru na kuwapima ng'ombe wote kabla ya kumfikia mlaji,"Peter Kasele,Afisa Mifugo.
Umoja wa wazee Mkoani Mwanza UWAMKOMWA ulioanzishwa rasmi Juni 15,2022 una wanachana hai 37 kutoka Wilaya zote 7 za Mkoa huo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.