Tumieni fursa zilizopo Mwanza kutanua wigo wa kazi zenu za usindikaji maziwa-RAS Balandya
Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza Ndg.Balandya Elikana amewashauri wasindikaji wa maziwa kutumia fursa zilizopo Mkoani humo ili kutanua wigo wa kazi zao ili wazidi kujiimarisha kiuchumi na kujihakikishia pato lao.
Akifungua kongamano la wadau wa tasnia ya maziwa kwa niaba yake, leo septemba 26, 2023 kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Katibu Tawala Msaidizi Seksheni ya uchumi na uzalishaji,Emil Kasagara amesema fursa za reli ya kisasa inayotarajiwa kukamilika mwakani, mgodi wa Nyanzaga na Daraja la JP Magufuli ni eneo ambalo ni mkombozi kwa wasindikaji kufanya kazi zao kwa uhakika.
"Ndugu zangu wadau mliohudhuria kongamano hili, sasa muanze kuangalia hatua ya kuwa na viwanda kutokana na uhitaji wa mzigo mkubwa kupita fursa zilizopo Mkoani Mwanza mkizingatia uzalishaji ulio bora ili muweze kumudu soko la ushindani",amesisitiza Kasagara.
Amesema kuna asilimia asilimia 30 ya hali ya udumavu kwa watoto wetu kutokana na ukosefu wa unywaji wa maziwa hali inayochangiwa na kushindwa kumudu vizuri masomo yao,hivyo kupitia jukwaa hilo la kongamano waje na matokeo chanya katika kuleta mapinduzi ya hali ya unywaji wa maziwa shuleni.
Awali akizungumzia lengo la kongamano hilo kuelekea kilele cha siku ya unyweshaji maziwa shuleni yanayofanyika Kitaifa Mkoani Mwanza,Msajili kutoka Bodi ya maziwa Tanzania TDB,George Msalia amebainisha wamekutana na wadau hao ili kubadishana uzoefu na kubaini changamoto zao ili kuzifanyia kazi na mwishowe kuwepo na tija katika unywaji wa maziwa shuleni.
"Hapa tuna wataalamu mbalimbali watakaowasilisha mada zikiwemo Taasisi za Fedha hasa kwa kutambua changamoto za mitaji kwa kutambua ni bidhaa inayohitaji mazingira safi na umakini usipokuwepo hasara ya kuharibika kwa haraka inajitokeza hivyo huduma za kibenki zina nafasi yake",Msalia.
"Hadi sasa tuna mikoa 8 inayotekelezwa mpango huu wa unyweshaji maziwa shuleni na tuna shule 134 mpango ni kufikia shule 5000," amefafanua Prof.Zacharia Masanyiwa Mwenyekiti wa Bodi ya maziwa Tanzania TDB
Kongamano hilo limewakutanisha pia walimu wa kutoka shule za Msingi na Sekondari ambapo mpango wa unyweshaji maziwa unatekelezwa shuleni kwao.
Aidha katika kuelekea kilele cha maadhimisho hayo wadau wa tasnia ya maziwa walitembelea shule kadhaa Mkoani Mwanza kutoka Wilaya za Nyamagana na Ilemela na kugawa maziwa kwa wanafunzi pamoja na kutoa elimu kuhusu umuhimu wa unywaji maziwa.
Kila Jumatano ya mwisho wa mwezi wa Septemba Tanzania inaungana na Mataifa mengine Duniani kuadhimisha siku ya unyweshaji maziwa shuleni ambapo Kitaifa mwaka huu yanafanyika Mkoani Mwanza Septemba 27,2023 kwenye viwanja vya Furahisha.
Kauli mbiu ya mwaka huu inasema "MPE MTOTO MAZIWA KWA MAENDELEO BORA SHULENI".
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.