Tumieni Jukwaa hili la mkutano wenu mkuu ili mje na maboresho zaidi katika sekta ya elimu nchini: Naibu Waziri Ndejembi
Naibu Waziri wa nchi Ofisi ya Rais,Tamisemi Mhe. Deogratius Ndejembi ameutaka umoja wa walimu wa shule za Sekondari nchini TAHOSSA kuutumia mkutano wao mkuu wa 18 unaofanyika Mkoani Mwanza kama jukwaa la kuleta mageuzi chanya katika sekta ya elimu nchini.
Mh.Ndejembi ametoa rai hiyo leo wakati akifungua mkutano huo kwenye ukumbi wa Malaika Beach Resort, amebainisha umoja huo ni chombo muhimu katika kuleta maendeleo hivyo yote yatakayojadiliwa kwenye mkutano huo yawe na tija kwa Taifa letu.
"Rais wetu ameonesha nia ya dhati ya kupigania maendeleo ya nchi yetu kwa kuboresha sekta ya elimu, wote ni mashuhuda wa fedha za Uvico19 zilivyo jenga madarasa bora nchini nzima, ni wajibu wetu sisi kumuunga mkono kwa vitendo ili kutimiza ndoto yake ya kuona Taifa linazidi kustawi kwa viwango bora vya elimu kwa wanafunzi," Naibu Waziri.
Amewahimiza wakuu hao wa shule kuendelea kuwa wafanyakazi wa mfano kama walivyoonesha wakati wa ujenzi wa madarasa yaliyokamilika kwa wakati, ubora unaokwenda na thamani ya fedha na weledi wa matumizi ya fedha zilizo kusudiwa.
Aidha katika Mkutano huo Mhe. Ndejembi alitoa maamuzi ya kiwanja cha TAHOSSA kilichopo eneo la Ihumwa, Dodoma kilicholengwa kama kitega uchumi chao, warejeshewe mara moja baada ya kupewa taasisi ya MKURABITA ambayo tayari imefutwa, alipompigia simu ya hadharani Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma na kumpa maelekezo hayo.
Awali akimkaribisha mgeni rasmi wa mkutano huo Katibu Tawala wa mkoa wa Mwanza,Ndg.Balandya Elikana amesema mwaka 2023-24 wamepokea jumla ya Shs bilioni 89.7 kwa ajili ya kuboresha miundombinu katika sekta ya elimu hali iliyochangia kuwa na madarasa bora na wanafunzi kusomea katika mazingira rafiki yasiyo na msongamano.
"Ndugu Naibu Waziri Ofisi ya mkuu wa mkoa imesimama imara kuhakikisha miradi yote iliyokusudiwa katika sekta ya elimu inakamilika kwa wakati na kwa ubora unaokwenda na thamani ya fedha,"amesema mtendaji huyo wa mkoa mbele ya wakuu wa shule za sekondari.
Rais wa TAHOSSA Dennis Otieno amesema katika siku tatu za mkutano wao watajadili mambo mbalimbali ya kuboresha elimu nchini ikiwemo kuzitambua na kuzipa zawadi maalum shule zinazofanya vizuri na zile zisizofanya vizuri kuona zinakabiliwa na changamoto gani ili kupata ufumbuzi.
Mkutano huo unatarajiwa kufungwa Disemba 17,2023 na Waziri wa nchi Ofisi ya Rais,Tamisemi Mhe.Mohamed Mchengerwa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.