UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA MWANZA UTAKUA WA AMANI : MTANDA
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda ametoa wito kwa viongozi wa dini mkoani humo kuendelea kuhamasisha wananchi kujiandaa kushiriki kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa ambao utakua huru kwani utazingatia sheria na kanuni za uchaguzi.
Ametoa wito huo leo Novemba 06, 2024 wakati akihutubia kongamano la viongozi wa dini kutoka kamati ya amani ya Mkoa wa Mwanza lililofanyika mahususi kuhamasisha upigaji kura kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa wa Novemva 27, 2024.
Ameongeza kuwa Mkoa wa Mwanza umejipanga kuhakikisha uchaguzi wa Serikali za mitaa unakua wa haki, uhuru na amani kwa kufuata sheria, kanuni, taratibu za uchaguzi na kwamba wananchi wanapaswa kujiandaa kushiriki bila hofu yoyote.
"Mkoa wa Mwanza tulilenga kuandikisha watu milioni 1.9 lakini tumeandikisha watu milioni 2.86 sawa na asilimia 106 na tumeshika mafasi ya 3 kwa mikoa , nawashukuru sana viongozi wa dini kwa hamasa yenu na nitaendelea kushirikiana nanyi kila siku."
Vilevile, amewataka wananchi kujiepusha na mizengwe ya uchaguzi na kutowekeana mapingamizi yasiyo na sababu baina ya chama kimoja na kingine na kwamba ni lazima wasimamizi wa uchaguzi huo wamtangaze mshindi mara moja bila kusubiri jambo lolote.
Sheikh wa Mkoa wa Mwanza Hassan Kabeke ambaye pia ni Mwenyekiti Mwenza wa Kamati ya amani amesema uchaguzi upo kwenye vitabu vya dini hivyo viongozi wa dini wanapaswa kuhakikisha wanahamasisha wananchi kushiriki tena kwa amani.
Mwenyekiti Mwenza Kamati ya Amani ya Viongozi wa dini Mkoa wa Mwanza Askofu Charles Sekelwa amesema demokrasia siyo haki tu ya kupiga kura bali pia nafasi ya wananchi baada ya kusikiliza sera kuamua ni nani wamchague kwani watakua wameshajua nini atawapatia.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.