Uhusiano baina ya Tanzania kichocheo cha kuinua uchumi-Balozi Chen
Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China nchini Tanzania Mhe.Chen Mingjian amesema Tanzania na China zitaendelea kufaidika na uhusiano mzuri ulioasisiwa na Baba wa Taifa Hayati Julius Nyerere na Mao Tsetung katika kuinua uchumi wa nchi hizo kupitia nyanja mbalimbali.
Balozi Chen amezungumza hayo leo Mkoani Mwanza akiwa na timu ya wabunge kumi kutoka Bunge la Tanzania ambao ni marafiki na Bunge la China mara baada ya kuhitimisha ziara yake fupi ya kutembelea miradi ya kimkakati inayotekelezwa na Kampuni ya kutoka nchini kwake ya CCECC inayojenga Daraja la JP Magufuli na mradi wa Reli ya kisasa SGR kipande cha tano kutoka Isaka kuja Mwanza.
Balozi Chen amesema Makampuni 17 kutoka China yapo nchini kutekeleza miradi mbalimbali ikiwa ni matokeo chanya ya mahusiano ya nchi mbili zenye mahusiano adhimu.
Ameongeza kuwa amefurahishwa kuona wataalamu kutoka Tanzania wanafanya kazi bega kwa bega kwenye mradi wa Daraja la JP Magufuli kwa lengo la kupata ujuzi zaidi ili kuja kuwa tegemeo katika miradi ijayo.
"Nchi yangu inanufaika sana kutokana na mahusiano mazuri tuliyonayo,tupo katika kujiimarisha na lugha ya kiswahili ili kufundisha kwenye vyuo vikuu vyetu na sehemu nyingine, watu kutoka China wapo hapa Tanzania kujipatia taaluma hiyo,"amesisitiza Balozi Chen.
Akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa urafiki wa Wabunge baina ya Tanzania na China Mhe.Dkt.Charles Kimei,Mbunge wa Masasi mjini Mhe.Geofrey Mwambe amesema mradi wa Daraja la JP Magufuli na Reli ya kisasa utakuwa kitega uchumi cha uhakika kutokana na Mwanza kuwa na jirani na nchi za maziwa makuu.
"Sina shaka yoyote na uwekezaji unaofanywa na China kwenye nchi yetu siku za nyuma nimekuwa Mtendaji Mkuu wa kituo cha uwekezaji nafahamu vizuri Tanzania tunavyonufaika,"Mhe.Mwambe.
Mradi wa Daraja la JP Magufuli uliyogharimu bilioni 716 unatarajia kukamilika Disemba mwakani wakati Reli ya kisasa SGR kipande cha kutoka Isaka hadi Mwanza wenye gharama ya zaidi ya Trilioni 3 utakamilika Mei mwakani.
Akiwa kwenye mradi wa SGR Wilayani Kishapu,Balozi Chen ametembelea kiwanda cha kufyatua mataluma ya Reli na kuzungumza na wafanyakazi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.