Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amewaasa Maafisa Tarafa na Watendaji wa Kata kuweka jitihada kwenye kazi zao kwa kuzikubali nafasi zao na kutekeleza majukumu yao kwa bidii ili waweze kuleta tija katika jamii wanazoziongoza.
Mhe. Mtanda ameyasema hayo leo tarehe 29 julai, 2025 wakati akiwahutubia Watendaji na Maafisa hao zaidi ya 300 kutoka katika Mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Mara, Simiyu, Geita, Tabora na Kagera walioajiriwa
Kuanzia Julai, 2024.
“Kazi yako ukiipenda utaifanyia juhudi, na ukifanikiwa hayo basi utajikuta umejiendeleza kielimu, kuweka weledi na nidhamu, kwa ujumla kuishi ndani ya utumishi huo kizalendo.” Mhe. Mtanda.
Aidha, amewataka kutumia taaluma zao kuonesha tabia njema kwa jamii inayowazunguka na kuonesha uwezo kwenye kazi zao na staha ya maisha kwenye maeneo yao ya uongozi.
Kadhalika, amewataka kwenda kufanya maamuzi sahihi yanayozingatia sheria, kanunu na miongozo iliyowekwa katika sekta husika mathalani ardhi na sio kufanya uonevu kwa kundi moja au jingine kwani hali hiyo uharibu kazi.
Vilevile Mkuu wa Mkoa amewataka kwenda kuwaunganisha wananchi na sio kuwagawanya pia kuhakikisha wanawajengea ari ya kujitolea kwa serikali yao hususani kwenye uanzishwaji wa miradi ya maendeleo kama ujenzi wa madarasa, miradi ya maji na barabara.
Hata hivyo, amewataka kuishi kuendana na mazingira watakayoyakuta kwa wananchi wanaoishi nao katika maeneo yao ya kazi na kuwa wabunifu mathalani waonapo vyanzo vya mapato vipya na kuviwasilisha kwenye Halmashauri ili vipitiwe na kuingizwa katika maoteo ya kodi na ushuru.
Katika mafunzo hayo washiriki wamejengewa uelewa wa kina kuhusu muundo na majukumu yao ya kikazi, sera na sheria za Serikali, mbinu za kusimamia miradi ya maendeleo, namna ya kushughulikia kero za wananchi kwa wakati, pamoja na usimamizi bora wa rasilimali na mapato ya ndani.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.