Upimaji wa Virusi vya UKIMWI waongezeka Mkoani Mwanza.Hayo yamebainishwa leo katika Maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani ambayo yamefanyika Kimkoa katika Viwanja vya Furahisha wilaya ya Ilemela.
Akiongea kwenye Maadhimisho hayo Mgeni rasmi Mhe. Dkt Severin Lalika amesema Upimaji wa VVU umeongezeka Zaidi katika Mkoa wetu kupitia kampeni iliyozinduliwa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza tarehe 21/07/2018 katika viwanja vya furahisha ambapo kwa siku hiyo peke yake watu 2006 walipimwa wanaume wakiwa 1,234 na wanawake wakiwa 772 na jumla ya watu 167 waligundulika kuwa na maambukizi ya VVU,wanaume 94 na wanawake 73
Aidha Halmashauri ziliendelea na Kampeni hiyo ya upimaji na kufanya jumla ya watu 714,842 kupima afya zao ,wanaume 252,539 na wanawake 462,303 ambapo kwa Idadi hiyo watu 8,197 waligundulika kuwa na maambukizi ya Virusi vya UKIMWI
Mhe.Dkt Severin amesema kutokana na Takwimu zilizopo zinazoonesha Maambukizi ya UKIMWI Mkoani Mwanza zimepanda kutoka Asilimia 4.2 mpaka Asilimia 7.2 kwa Mwaka 2016/17 hivyo kuwataka wananchi pamoja na wadau mbalimbali kuendelea kuunga mkono Jitihada zinazofanywa na wananchi pamoja na wadau mbali mbali za kupunguza maambukizi ya Virusi vya UKIMWI
Akitoa Salamu za Nyamagana Mkuu wa wilaya ya Nyamagana Dkt.Phillis Nyimbi amesema kutokana na takwimu za maambukizi ya Virusi vya UKIMWI,Nyamagana imeonekana inaongoza kuwa na Idadi Kubwa ya maambukizi ambapo watu 23,583 wamegundulika kuwa na Virusi vya UKIMWI“Mimi kama msimazi mkuu wa wilaya ninalichukua hili na kwenda kuwashirikisha viongozi wengine wilayani kwangu na kulifanyia kazi” amesema Dkt Nyimbi
Aidha Dkt Nyimbi amewataka wadau mbali mbali wanaojishughulisha na shughuli za Afya kufika Ofisini kwake nayeye yupo tayari kutoa ushirikiano kupunguza kiwango hicho cha maambukizi
Akisoma Taarifa ya Maambukizi ya UKIMWI kimkoa Mratibu wa UKIMWI Mkoa Dkt Pius Masele amesema kwa Takwimu za Mwaka 2017 /18, Mwanza umekua Mkoa wa Nne kitaifa kuwa na Idadi kubwa ya maambukizi ya Virusi vya UKIMWI ambapo kiwilaya Nyamagana ikishika nafasi ya Kwanza kuwa na Idadi ya watu 23,583 walioambukizwa VVU
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.