Utapiamlo bado ni changamoto kwenye vituo vya kulea watoto nchini: Katibu Mkuu SMZ
Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Wanawake, Wazee na Watoto kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) Abeida Abdallah amesema bado inahitajika nguvu ya wadau wa maendeleo kukabiliana na changamoto ya utapiamlo kwa watoto wanaolelewa kwenye vituo mbalimbali nchini.
Akizungumza na wafanyajazi kwenye kituo cha Anza kwa Imani kilichopo wilayani Misungwi Mtendaji huyo mwandamizi wa Wizara amesema utapiamlo bado ni tatizo hivyo amewaomba wadau na wananchi wenye uwezo kusaidia upatikanaji wa mahitaji kwa watoto ikiwemo chakula, mavazi na matibabu.
"Natoa wito Serikali tunahudumia, lakini pia wananchi ambao wanauwezo wajitokeze kusaidia vituo ili watoto wapate lishe bora" amesema Bi. Abeida.
Katika ziara yake fupi Mkoani Mwanza Katibu Mkuu huyo ametembelea makao ya wazee wasiojiweza yaliyoko Bukumbi wilayani Misungwi na kutoa Rai kwa wazee hao kuendelea kutunzwa ili waepukane na magonjwa nyemelezi huku akisisitiza ulaji wa mlo kamili pamoja na matumizi ya mboga za majani kwa wingi ili kulinda afya zao ambao ni tunu kubwa katika Taifa.
Aidha, Katibu Tawala Msaidizi Utawala na Rasilimali Daniel Machunda akimuwakilisha Katibu Tawala wa Mkoa huo amempongeza Katibu Mkuu huyo kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (smz) kwa kuuchagua Mkoa wa Mwanza kuja kutembelea makao mbalimbali ya watoto pamoja na makao ya wazee Bukumbi ambapo amesema Serikali ya mkoani humo inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo kuhakikisha vituo vya watoto pamoja na makao ya wazee Bukumbi wanapata mahitaji stahiki ikiwemo mavazi na chakula.
Naye Grace Chenya ambaye ni Afisa Ustawi Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi maalumu amebainisha Serikali inaendelea kusimamia na kuhakikisha watoto wanapata malezi bora ikiwemo huduma za afya na elimu.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.