Zoezi la ugawaji vyandarua bure kwa wanafunzi wa shule za msingi Mkoani Mwanza limezinduliwa rasmi oktoba 10 mwaka huu ambapo jumla ya vyandarua 445,254 vinategemea kugawiwa.
Akifungua zoezi hilo wakati wa hafla fupi iliyofanyika katika shule ya msingi Nyanza mkoani hapa, Mkuu wa Mkoa Mhe.John Mongella amesema kuwa ugawaji wa vyandarua hivi ni ishara ya kuendelea kwa mapambano dhidi ya ugonjwa wa malaria.
"Kama mnavyojua Ugonjwa wa malaria bado umeendelea kuwa tishio kwa kina mama na watoto na hata wanume pia, leo tupo hapa kuanza rasmi ugawaji wa vyandarua kwa wanafunzi wa shule za msingi mkoani kwetu.
"Tumeamua kuanza na watoto wa shule za msingi kwa sababu hawa ndiyo watu wazima wa kesho hivyo tukiwajengea utamaduni wa matumizi sahihi ya vyandarua itajengeka kuwa tabia yao kumbe wataendeleza hata watakapokuwa na maisha yao ya kujitegemea.
"Mpaka sasa takwimu zinaonyesha kuwa maambukizi ya malaria kitaifa yameshuka hadi asilimia saba huku sisi kama Mkoa tuna asilimia nane na hii inaonyesha wastani wetu upo juu zaidi ya wastani wa taifa.
"Hivyo niwaombe tuendelee kushirikiana sote kwa pamoja ili baada ya miaka kadhaa ijayo tuwe tumefikia asilimia sifuri na nina amini inawezekana kama kila mmoja atakubali kuweka nguvu zake kuhakikisha tunatokomeza ugonjwa huu,"alisema Mongella.
"Niwaagize viongozi wote kuanzia ngazi ya Mkoa hadi ngazi ya shule kuhakikisha zoezi hili linasimamiwa kikamilifu ili vyandarua hivi viweze kugawiwa kwa madarasa yaliyokusudiwa bila upendeleo na mwisho wa siku kuwe na matokeo chanya katika kutokomeza malaria,"alisema Mongella.
Awali akisoma taarifa fupi juu ya mwenendo na matarajio ya zoezi hilo Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa, Tuloson Nyalanja alisema kuwa mpango wa ugawaji vyandarua hivi ni endelevu na unategemewa kuwa chachu ya kuzima ugonjwa wa malaria Mkoa wa Mwanza na Tanzania kwa ujumla.
"Zoezi hili mwaka huu linafanyika kwa awamu ya nne mfululizo ambapo lilianza rasmi mwaka 2016 na mpaka sasa limekuwa na manufaa ingawa bado kuna changamoto ya matumizi sahihi ya vyandarua.
"Kama ilivyo kawaida yetu tumelenga kuzifikia shule zote 976 mfululizo zilizopo kwenye halmashauri nane za Mkoa wa Mwanza ambapo tutawagawia vyandarua wanafunzi wote wa darasa la tatu hadi la sita kwa muda wa wiki mbili.
"Mbali na kugawa vyandarua lakini kwa Mwaka huu tumewekeza nguvu zaidi kutoa elimu ya matumizi sahihi ya vyandarua kwa kila atakakayepokea chandarua ili kuhakikisha kuwa tunafanikiwa kwa kiwango kikubwa.
"Niwaombe wanafunzi, wazazi na walezi kuzingatia elimu ya matumizi sahihi ya vyandarua ili kwa pamoja tufanikishe adhima ya kupunguza maambukizi kutoka asilimia nane hadi zero kwa mkoa na sisi kama ofisi ya mganga mkuu mkoa tutahakikisha tunapita mitaani kufuatilia matumizi sahihi ya vyandadua hivi," alisema Nyalanja.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Wilaya ya Nyamagana Yonas Alfred akizungumuza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya hiyo ambapo ndiyo zoezi hilo limeanzia amewaomba wakazi wa wilaya ya Nyamagana na Mwanza kwa ujumla kuunga mkono na kuzingatia elimu ya matumizi sahihi ya vyandarua inayotolewa kwa wanafunzi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.