Katika kuhakikisha vijana wanajikwamua kiuchumi na kuondokana na tatizo la ajira jumla ya vijana 181 wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela wamenufaika na mradi wa vijana na mkwanja.
Mradi huo wa miaka mitatu ulioanza 2019 hadi 2021,unaotekelezwa na shirika la Mtandao wa Vijana na Watoto Mwanza (MYCN) kwa ufadhili wa The Foundation for Civili Society ambao umegharimu jumla ya milioni 79.
Akizungumzia jijini Mwanza Ofisa Miradi wa MYCN Generosa Ladislaus, amesema mradi huo unatekelezwa katika Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela ambapo inahusisha jumla ya kata sita(6) ikiwemo Buswelu,Nyasaka, Ilemela,Shibula,Kitangiri na Nyamanoro.
Generosa amesema,lengo kuu la mradi huo ni kuwakwamua vijana kiuchumi ndani ya manispaa hiyo hususani kwa kuhakikisha vijana wajasiriamali wanapata fursa za masoko,kujikwamua kimaisha,kumiliki mali na rasilimali.
" Vijana 181 wameweza kufikiwa moja kwa moja katika kipindi cha mwaka wa utekelezaji ikiwa vijana wa kike 93 na wakiume 88,huku jumla ya vijana 1420 wamefikiwa kwa njia ya mitandao ya kijamii,redio na vipindi vya televisheni hivyo kufanya jumla ya vijana 1,601 kufikiwa," amesema Generosa.
Pia amesema,vijana wameweza kuanzisha biashara mbalimbali ikiwemo utengenezaji na uuzaji wa unga lishe,siaga ya Karanga,mvinyo wa zabibu na rozela,viungo vya chakula na chai,unga wa soya,majani ya chai,mafuta ya kujipaka mwilini na kwenye nywele,vikapu na viti ,sabuni za maji ,batiki,ufugaji wa kuku,uuzaji wa kuku na nafaka pamoja na uuzaji wa urembo na nguo.
Aidha amesema, miongoni mwa changamoto zilizojitokeza wakati wa kutekeleza mradi huo ni pamoja na taratibu za upatikanaji wa vibali vya uthibiti ubora,mashine za uzalishaji na vifungashio pamoja na mlipuko wa virusi vya Corona(COVID-19) ambao umechangia kikwamisha ufikiwaji na uhusishwaji wa idadi kubwa ya vijana.
Mkurugenzi Mtendaji wa MYCN Brightius Titus, amesema mradi huo umegharimu milioni 79 ambapo umetekelezwa kwa awamu mbili ambapo awamu ya kwanza uligharimu milioni 40 ulitekelezwa kwa miezi 6 Julai hadi Desemba 2019 huku awamu ya pili ambayo ilitumia milioni 39 ilianza Julai 2020 hadi Machi 2021.
Titus amesema,waliamua kuja na mradi huo baada ya uwepo wa vijana kushindwa kuendelea na masomo pamoja na wimbi la ukosefu wa ajira,kwanza walihakikisha vijana wanapata elimu ya utambuzi,kuwafundisha namna gani watatumia rasilimali za ndani kulingana na maeneo yaliyopo kisha wakawapeleka SIDO kupata mafunzo ya uzalishaji na masoko huku Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela ikawapa mitaji vikundi vitano kati ya sita kupitia mikopo ya asilimia 4 ya vijana inayotolewa na Halmashauri ili kufanya shughuli za uzalishaji.
"Kilicho tusukuma sisi kuja na mradi wa vijana na mkwanja ni ukitizama takwimu zinaonesha vijana wengi nchini Tanzania wanakabiliwa na wimbi la ukosefu wa ajira kwaio wanaishi katika wimbi kubwa la umasikini,wakaona moja ya kipaumbele cha vijana kujikwamua ni kuwawezesha kiuchumi na tunategemea kuingia awamu ya tatu ya mradi huu ambao utaenda kwa muda wa miaka mitano,"amesema Titus.
Pia amesema,matokeo chanya ambayo yamepatikana ni vijana wameweza kujiajiri kwani wapo walioanzisha viwanda vidogo vya ufyatuaji matofali,usindikaji wa nafaka,huduma ya chakula na wengine wanafanya ufugaji wa kuku ambao wanafikia takribani mia tano ambapo wamebadilika kiuchumi na baadhi yao wameanza kujenga.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.