Mkuu wa idara ya miundombinu Mkoa wa Mwanza Mhandisi Chagu Ngh'oma amesema uwepo wa vikao kazi katika eneo la ujenzi wa hospitali ya rufaa yenye hadhi ya Mkoa inayojengwa wilayani Ukerewe vimesaidia kubaini na kutatua changamoto ambazo zingepelekea kuchelewesha ujenzi.
Amesema hayo mapema leo jumamosi julai 19, 2025 katika kikao kazi cha 4 kilichofanyika kwenye eneo la ujenzi kijiji cha Bulamba ambapo amebainisha kuwa kupitia vikao hivyo mkandarasi aliwasilisha changamoto mbalimbali ambazo ofisi ya Mkuu wa Mkoa imezitatua.
Pamoja na Mkandarasi kulipwa fedha stahiki kwa mujibu wa mkataba kulingana na hatua ya ujenzi iliyofikiwa, ametaja adha ya kusafirisha kokoto kutoka Mwanza na uwepo wa chemchem ya maji katika eneo la ujenzi amesema kuwa zilibainika na kwa ushirikiano na mkandarasi huyo zimeshatatuliwa.
Akizungumza baada ya timu ya ufuatiliaji huo kukagua ujenzi Mhandisi Ngh'oma amemtaka mkandarasi huyo kuongeza kasi ya ujenzi na hadi kufikia Agosti 02, 2025 awe ameezeka majengo ya kusubiria, kuhifadhi maiti pamoja na jengo la kupokelea umeme na kwa jengo kuu wawe wameshamaliza kuweka vitako 3 vilivyobaki kukamilisha 188.
Naye, Kaimu Mganga Mkuu Mkoa huo Dkt. Silas Wambura amebainisha kiu ya wananchi wa Kisiwa hicho pamoja na vingine 38 wanaosubiri huduma za kibingwa na akatoa rai kwa mkandarasi kuongeza rasilimali watu kwenye ujenzi huo ili akamilishe ujenzi kwa wakati na huduma ziweze kutolewa.
Timu hiyo ya ufuatiliaji kwa kupitia kikao kazi hicho cha 4 imebaini ucheleweshaji wa kazi kwa zaidi ya miezi mitatu katika kufikia malengo aliyopewa mkandarasi mzawa Dimetoclasa Realhope Limited anayetekeleza mradi huo wenye thamani ya zaidi ya Tshs. Bilioni 25 ambao umeanza tarehe 10 januari, 2025 na unatarajiwa kukamilika Julai 08, 2026.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.