Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Adam Malima ameziagiza halmashauri zote zilizopo mkoani humo kutoa mafunzo kwa Viongozi wa umma ili kuwakumbusha kutenda kazi kwa kuzingatia sheria, kanuni, maadili na uadilifu wa utumishi wa umma.
Mhe. Malima amesema kumekuwa na mmomonyoka mkubwa wa ukiukwaji maadili kwa baadhi ya watumishi wa umma wanapotekeleza majukumu yao ikiwemo miradi ya maendeleo hali inayosababisha itekelezwe chini ya kiwango ikiwa haina thamani halisi ya fedha.
Mhe. Malima ameyasema hayo leo Mei 5, 2023 wakati akifungua mafunzo ya maadili kwa viongozi wa umma wa Mkoa wa Mwanza yaliyolenga kuwakumbusha viongozi na wakuuu wa taasisi za umma mkoani humo kuzingatia kanuni, sheria na taratibu wakati wa kutekeleza majukumu yao, kujiepusha na masuala yote yanayoweza kuwaingiza kwenye mgongano wa maslahi na kuzingatia suala la uwajibikaji wa pamoja.
“Maadili ni nguzo muhimu sana katika kufanikisha mipango ya maendeleo, viongozi wa umma zingatieni hilo hasa zile Taasisi zinazotekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kwa manufaa ya wananchi kwa mfano MWAUWASA, TARURA, RUWASA, TANESCO na REA mnapokosa uadilifu mkakoroga mradi anayetukanwa na wananchi ni Mhe. Rais na Chama cha Mapinduzi wakati lengo la Serikali ni kuinua maisha ya wananchi kiuchumi ndani ya mkoa wa Mwanza sitawavumilia”amesema Mhe. Malima.
Naye, Katibu Msaidizi wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Kanda ya Ziwa, Godson Kweka, amesema mafunzo hayo yana mada tatu ambazo ni Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma ambapo wanakumbushana misingi ya Maadili ya Umma kama ilivyoainishwa kwenye Sheria hiyo, mgongano wa maslahi na Uwajibikaji wa pamoja katika kuwaletea wananchi maendeleo.
“Tunawakumbusha Viongozi wa Umma Mkoa wa Mwanza kuishi na kuheshimu viapo vyao vya ahadi ya uadilifu walivyoapa kwa nyakati tofauti walipopewa dhamana ya nafasi walizonazo kwa sasa kipaumbele kikubwa cha sekretarieti ya maadili ya umma pamoja na mambo mengine ni kuhimiza suala zima la uwajibikaji wa pamoja kwa viongozi, watumishi na wananchi katika ushirikishwaji ili kuwaletea wananchi maendeleo,”amsesema na kuongeza.
“Sisi sote ni mashahidi, hatuna shaka na tunakila sababu ya kumpongeza Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jinsi anavyotafuta fedha za kutekeleza miradi mbalimbali katika halmashauri zetu kwa ajili ya kuwaletea wananchi maendeleo miradi hiyo inahitaji kuwa na viongozi waadilifu kwenye usimamizi wa fedha na usimamizi wa rasilimali zingine ambazo zipo kwenye maeneo yao ya kazi.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Balandya Elikana, amewataka watumishi wa umma kufanya kazi kwa uadilifu na kuwa wazalendo ili kukidhi matarajio ya wananchi kwa serikali yao katika kuwaletea maendeleo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.