*Viwanja vya Shule vyatakiwa kupanuliwa kusaidia Ujenzi wa Miundombinu*
Halmashauri ya wilaya ya Ukerewe imekamilisha Ujenzi wa vyumba vya Madarasa 76 vyenye thamani ya Bilioni 1.52 kwa ajili ya wanafunzi 10439 waliofaulu kujiunga na Kidato cha kwanza 2023 ambao wanaendelea kusajiliwa kwa ajili ya kuanza Mwaka wa masomo.
Akiongea na wananchi kwenye hafla ya makabidhiano iliyofanyika kwenye shule ya Sekondari Mumbuga, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Adam Malima ametoa wito kwa viongozi wa Wilaya zote Mkoani humo kuweka mpango wa kuongeza maeneo kwenye Shule zote zenye maeneo finyu ili kuwa na eneo la kujenga Miundombinu mingine siku za baadae.
"Madarasa haya 76 ni miongoni mwa 980 yaliyojengwa Mkoani Mwanza nasi ndio tumeongoza kwa kupata fedha nyingi za Ujenzi nchini, tunamshukuru sana Mhe. Rais kwa sababu ametujali na tutanufaika sana na miundombinu hii, nawasihi tulipe wema kwa wema na kipekee tuhakikishe tunawaleta watoto shule." Amesema Malima.
Aidha, ametoa wito kwa viongozi wa Halmashauri hiyo kukamilisha Maboma ya Madarasa kwenye shule zote ili kuunga mkono juhudi za wananchi walioanzisha Ujenzi kwa kujitolea nguvukazi na katika kuhamasisha hilo Mhe. Malima amechangia Mifuko 40 ya Saruji.
"Madarasa haya hayatakua na maana kama watoto hawatakuja kusoma hivyo nawaomba tuhamasishane wazazi, walezi na wadau wote kuwaleta wanafunzi wote waliochaguliwa kuja kujiunga kidato cha kwanza mapema iwezekanavyo." Amesema Katibu Tawala Mkoa.
Kanali Denis Mwila, Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe amemshukuru Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwaletea fedha za kujenga Madarasa hayo pamoja na utengenezaji wa seti za Viti na Meza 3800.
"Mbinu ya kufanya manunuzi kwa pamoja (Bulk purchase) imesaidia kupata vifaa vya Ujenzi kwa gharama za chini na utengenezaji wa seti meza na viti 3800 umefikia asilimia 98 na ifikapo Januari 18, 2023 zoezi hilo litakua limekamilika ikiwa ni pamoja na kufikisha Samani hizo kwenye shule zote." Emmanuel Sherembi, Mkurugenzi wa Halmashauri Ukerewe.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.