Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Adam Malima amewataka Waandishi wa Habari kutumia vyombo vyao kufikisha taarifa sahihi kwa wananchi hususani ujumbe wa masuala ya Afya ili kuwe na uelewa wa pamoja kwa mambo mbalimbali nchini.
Ametoa wito huo leo Agosti 18, 2022 wakati akifungua Semina ya mafunzo ya Uviko 19 kwa Waandishi wa Habari inayoratibiwa na Chama cha Waandishi wa Habari Mkoani humo kwa kushirikiana na Serikali kupitia Idara ya Afya ikilenga kuhamasisha chanjo ya ugonjwa huo kwenye jamii.
Mhe. Malima amebainisha kuwa kufikia Disemba 2022 Mkoa huo umelenga kuwafikia wananchi Milioni 2 wenye umri wa zaidi ya Miaka 18 kwa kuwapatia Chanjo ya Uviko 19 kupitia dozi rasmi zinazotolewa na Serikali hapa nchini.
"Ninayo taarifa ya mchango Mkubwa wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Mwanza kwenye Uhamasishaji wa Chanjo ya Uviko 19 kuanzia Uzinduzi na kampeni nzima ya kuhamasisha namna bora ya kuenenda ili kujikinga na maambukizi na hata kupambana na Matumizi ya dawa za kulevya, nawapongeza sana." Mkuu wa Mkoa.
Mwakilishi wa Muungano wa Klabu za Waandisbi wa Habari Tanzania (UTPC) Bi. Hilda Kileo amesema umoja huo unaendelea kuvilea vyama vya waandishi wa Habari Nchini na kwamba wanashirikiana na Serikali katika kuhakikisha jamii inapata Habari zilizo sahihi wakati wote.
Naye, Mwenyekiti wa Kilabu ya Waandishi wa Habari Mwanza, Edwin Nsoko amemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa ushirikiano na amebainisha kuwa vyombo vya habari ni rafiki wa serikali na daraja la maendeleo nchini hivyo wataendelea kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kama mlezi wa chama hicho.
Aidha, Ndugu Nsoko amebainisha kuwa chama hicho ni mabalozi hodari kwenye kufikisha ujumbe wa Chanjo ya Uviko 19 kwa wananchi ili jamii itambue umuhimu wa chanjo hii kwa maslahi mapana ya afya zao na ustawi wa Taifa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.