Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila, amesema njia pekee ya kusaidia jamii ni kufungamanishwa kwa shughuli za kiuchumi na biashara ya madini ili kuepuka jamii kuendelea kuwa masikini baada ya madini kuisha ardhini.
Alitoa kauli hiyo wakati akifungua Mkutano wa 14 wa Kimataifa wa Sekretarieti ya Ukaguzi ya Jumuiya ya Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR), unaofanyika jijini Mwanza, ukishirikisha nchi kumi na mbili.
Alisema bila kufungamanisha shughuli zingine za kiuchumi na biashara ya madini baada ya madini kuchimbwa na kuisha, wananchi na jamii wataendelea kubaki masikini na muafaka ni kuwawezesha watengenezaji wa vitona kuyaongeza thamani madini yanayozalishwa ili kuuza mazao ya madini hayo nje ya nchi badala ya kuuza madini ghafi.
“Shughuli za uchimbaji wa madini zinazofanyika ni wazi yakichimbwa yataisha na jamii itabaki maskini.Tuwawezeshe wachimbaji wadogo kukua na masonara, tukiliweza hilo tutakuwa na manufaa na hata yakiisha uchumi utabaki maana wachimbaji wadogo wakikua uchumi nao utakua,”alisema.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini alieleza kuwa wizara inakamilisha utaratibu wa vibali vya kusafirisha madini nje ya nchi uliowekwa na nchi wanachama wa Nchi za Maziwa Makuu ambapo awali yalisafirisha bila kufuata utaratibu kwa sababu ya changamoto ya kushindwa kufanya ukaguzi wa madini na kutoa taarifa na kuyasafirisha.
“Kila nchi inatakiwa kukamilisha utaratibu wa utoaji vibali vya usafirishaji ili madini yanaposafirishwa nje yaambatanishwe na cheti cha ukaguzi migodi, wapi yanatoka, ukaguzi wa migodi kama inakidhi vigezo na kudhibiti utoroshaji madini.Lengo ni kuwawezesha wanachama kushirikiana kuhakikisha madini hayatumiki kugharamia vita (matukio ya umwagaji damu),”alisema Profesa Msanjila.
Alidai matukio ya utoroshaji madini yamepungua na kwa kipindi cha mwezi mmoja kiasi cha kilo 500 za madini ya dhahabu imeuzwa mkoani Geita,ambayo ndiyo ilikuwa ikitoroshwana kwenye machimbo ya Tanzanite sh. bilioni 2.2 zimepatikana kutoka sh. milioni 700 kwa mwezi.
Naye Katibu Mtendaji wa Sekretarieti ya ICGLR, Balozi Zachary Muburi-Muita alisema mkutano huo unalenga kuwa na mikakati na nguvu ya pamoja, kumaliza vita na kusaidia kukuza uchumi wa nchi wanachama kutokana na vita ya kugombea utajiri wa madini, ikiwemo ya kiuchumi ya madini kutoroshwa bila kuwanufaisha wananchi.
Alisema utoroshaji wa madini bado ni tatizo na haujapungua licha ya wanachama kukabiliana na uchimbaji haramu, hivyo kwa kushirikiana na serikali ili kuweka nguvu ya pamoja, wananchi wapate tija kupitia madini na kushauri lugha ya Kiswahili itiliwe mkazo kwenye biashara na sera ya madini ya nchi wanachama wananchi waelewe zaidi.
“Tunataka kupata maendeleo ya kiuchumi baada ya kumaliza changamoto ya uvunaji na utoroshaji madini bila vibali.Tumepiga hatua ni wapi tunapaswa kujifunza.Mfano DRC vita dhidi ya serikali, vikundi hivyo nguvu yao inatokana na uvunaji haramu wa madini, vikiyakosa vitanyimwa nguvu hiyo,”alisema Balozi Muita.
Kwa upande wake David Luhaka kutoka Kalemi nchini DRC alieleza kuwa serikali ya nchi hiyo ilidhibiti usafirishaji wa madini nje bila vibali isipokuwa kwa njia halali kwani wanunuzi baadhi wan je walinunua madini kwa bei ndogo.
Alishauri kuwa makubaliano yaliyowekwa na nchi wanachama yanapaswa kuheshimiwa kwa sababu ni vigumu nchi moja kudhibiti usafirishaji madini nje bila kushirikiana, zikishirikiana kudhibiti uchimbaji na usafirishaji haramu zitakuwa na amani ya kudumu.
“ DRC ni tajiri wa madini mengi ambapo serikali ilidhibiti yasisafirishwe na tunaunga mkono vita hii ya utoroshaji madini.Serikali yetu haina siri, kulikuwepo fujo na vita, wavamizi waliyakalia maeneo ya madini na kuchimba, wizi na watu kufanya magendo na kuuza nje. Tumekubaliana na majirani Tanzania, Rwanda na Burundi (zote ni tajiri kama DRC ),ziishi kwa amani,”alisema Luhaka.
Kwa mujibu wa Luhaka DRC imejizatiti kuhakikisha biashara ya madini kwa magendo haifanyiki bali yasafirishwe kwa njia halali na kusifanyike makosa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.