Katika kusimamia na kuboresha ubora wa elimu na kiwango cha ufaulu nchini,Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza iliandaa kikao kilichowakutanisha wadau wa elimu kutoka Taasisi za serikali na zisizo za serikali ili kutoa ya moyoni na kujadili juu ya ubora wa elimu na kiwango cha ufaulu mkoani mwanza.
Akitoa taarifa ya maendeleo ya elimu mkoani Mwanza, Afisa Elimu wa Mkoa Michael Ligola alisema kuwa, kwa mujibu wa Takwimu za elimu kuanzia mwaka 2016 hadi 2018 zinaonyesha, Mkoa wa Mwanza kushuka Kitaifa kutoka nafasi ya 6 mwaka 2016, hadi nafasi ya 8 mwaka 2017 na nafasi ya 6 kwa mwaka 2018 kwa shule za msingi.
Ligola alisema, kwa upande wa shule za sekondari mkoa ulishika nafasi ya 6 mwaka 2016, nafasi ya 5 mwaka 2017 na nafasi ya 13 kwa mwaka 2018, hivyo kuonyesha wazi kuwa hakuna muendelezo kwa mkoa kuendelea kushika nafasi za juu kitaifa kila mwaka.
Alisema, takwimu zinaonyesha kuwa tatizo la wanafunzi kukatisha masomo na kuacha shule limeendelea kuwepo hasa kwa shule za msingi, ikiwa jumla ya wanafunzi 2646 wametajwa kutoendelea na masomo kwa sababu mbalimbali ikiwemo watoto wa kike 103 walioacha masomo kwa sababu ya mimba, wanafunzi 107 wakiacha shule kwa sababu ya magonjwa, huku wengine wakiacha shule kwa sababu tofauti tofauti ikiwa pamoja na utoro, vifo na utovu wa nidhamu.
Awali akifungua kikao hicho mkuu wa mkoa wa Mwanza Mhe. John Mongela aliwakumbusha wadau kutambua kuwa "Kipimo cha Elimu ni Mtihani" na hivyo kushuka kwa nafasi ya mkoa kitaifa kwa matokeo ya mtihani wa shule za msingi na sekondari ni kiashiria kuwa ubora wa elimu ki-mkoa unashuka na hivyo kuwaomba wadau wote wa elimu kuepuka kuleta siasa kwenye mjadala wa elimu na badala yake wang'amue changamoto zote.
Mhe.John Mongela aliwataka ,wasimamizi wa elimu Mkoa kufanya mapitio, usimamizi, na mijadala juu ya maazimio ya wadau katika kutimiza majukumu na uwajibikaji kwakuwa Mapinduzi ya Viwanda yanategemea elimu, hivyo misingi ya elimu ikiwa dhaifu mapinduzi ya sayansi na teknolojia hayawezi kufanikiwa.
Kwa upande wake Mdhibiti Mkuu Ubora Shule kanda ya Ziwa, Ndg Victor G Bwindiki alieleza kuwa ofisi yake imebaini changamoto mbalimbali kwa wanafunzi mashuleni ambazo huenda zinachangia kwa namna moja au nyingine kushusha kiwango na ubora wa elimu.
Bwindiki alisema, karibu shule zote zilizofanyiwa tathimini ya jumla hazikuwa na majengo muhimu kama vile majengo ya utawala na maabara.
Aidha kulikuwa na upungufu wa matundu ya vyoo na vyumba vya madarasa. Mbali na hayo taarifa imebaini uwepo wa tatizo la upungufu wa samani za waalimu na wanafunzi pamoja na mimba kwa wototo wa kike. Tatizo ambalo limeendelea kuondoa mazingira rafiki ya kujifunzia kwa wanafunzi na hivyo kuchangia kushusha kiwango cha ufaulu mkoa.
Akiongea kwa niaba ya wamiliki wa shule binafsi, mwenyekiti wa umoja wa wamiliki wa shule binafsi Tanzania (TAPEI) mkoa wa mwanza, Ndg, Raulent Samike aliiomba ofisi ya mkuu wa mkoa na serikali kwa ujumla kutatua changamoto zinazozikumba shule binafsi ikiwemo kutengwa kwenye maboresho ya mitaala, kuwepo mchakato mrefu wakati wa uanzishaji, uwepo wa Tozo zisizozingatia ukubwa wa shule, lakini pia aligusia suala la wanafunzi toka shule binafsi kukosa mikopo ya elimu ya juu.
Samike alisema kuwa siri kubwa ya shule binafsi kufanya vizuri ni pamoja na usimamizi mzuri, uwiano kati ya waalimu na wanafunzi, kuwepo kwa chakula mashuleni na miundombinu bora inayotoa mazingira rafiki ya kujifunzia kwa wanafunzi na waalimu na hivyo kuishauri serikali kuiga mfumo wa uendeshaji wa shule binafsi ili kufanikisha malengo ya kitaifa na kuinua kiwango cha elimu.
Nayo Taasisi ya Elimu ya watu wazima (EWW)-Mwanza kupitia kwa Ndg Chandale kachale ( mkufunzi mkuu EWW-,Mwanza) imesema, kwa kuwa taasisi hii imetoa mchango mkubwa kitaifa katika kutoa elimu kwa umma, kuna haja ya serikali kufanyia maboresho taasisi hii ikiwemo kuhakiki vituo vinavyotoa elimu ya watu wazima pamoja na waajili wake ili kurasimisha zaidi usimamizi wa elimu hii.
Uongozi wa vyuo vya ufundi (VETA), umeishauri jamii ya wakazi wa kanda ya ziwa na Tanzania kwa ujumla kufuta mitazamo hasi juu ya mafunzo ya ufundi kuwa anayepaswa kusoma vyuo hivyo ni yule aliyefeli na badala yake kuwataka wachangamkie fursa ya vyuo vya ufundi stadi (VETA) hasa katika kipindi hiki cha Tanzania ya viwanda.
Nao viongozi wa dini hawakuwa nyuma katika kutoa mchango wao juu ya maendeleo ya elimu. Akiwakilisha umoja wa makanisa ya kikristo Tanzania (CCT) mkoa wa mwanza, mchungaji Kepha Mlungu ambaye ni katibu wa CCT-mwanza, aliomba kuwepo na mikakati ya kila wilaya kuwa na angalau shule moja ya bweni kwa shule za sekondari ili kupunguza tatizo la watoto wa kike kupata ujauzito.
Aliwataka, wazazi na viongozi wa dini kufundisha maadili na hofu ya Mungu kwa watoto wa shule za msingi na sekondari ili kupunguza tatizo la mmomonyoko wa maadili, tatizo ambalo linachangia kwa kiasi kikubwa kuzorota kwa elimu.
Akimuwakilisha, Wakala wa Maendeleo ya Elimu Mkoa wa Mwanza Ester Jonas, alisisitiza ili kupata maendeleo endelevu ya elimu, ni vyema kuwepo na mipango imara katika usimamizi bora na endelevu wa elimu.
Akifunga Kikao hicho, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe.John Mongela aliwataka wakuu wa wilaya kuanzisha vikao vya wadau wa elimu kuanzia ngazi ya kijiji na kata ili kueleweshana sera na miongozo ya elimu huku akiwasisitiza viongozi wa elimu ngazi ya wilaya kutoa nafasi kwa wadau wenye uzoefu katika mijadala ya maendeleo ya elimu.
Pia aliwataka wakuu na wasimamizi wa elimu ngazi zote mkoa wa mwanza, kuiga mfumo wa usimamizi wa shule binafsi ili kufanikisha dhamira ya uwajibikaji.
Mhe. Mongella pia aliwahimiza maafisa elimu kutokaa maofsini muda wote na badala yake wazunguke kukutana na wananchi kwenye maeneo yao ya usimamizi ili kujua changamoto mbalimbali pamoja na kupokea maoni ya maboresho ya sera ya elimu.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.