WAELIMISHAJI JAMII MWANZA WANOLEWA USAFIRI WA M-MAMA
Mganga Mkuu Mkoa wa Mwanza Dkt. Jesca Lebba leo Julai 12, 2024 amefungua kikao kazi cha kuwajengea uwezo Waelimishaji jamii ngazi ya Mkoa na Halmashauri kuhusu usafiri wa dharula kwa Mama na Mtoto Mchanga (M-MAMA) chini ya ufadhili wa Pathfinder.
Akifungua kikao hicho Dkt. Lebba amewataka waratibu wa afya ya Mama na Mtoto, waratibu wa elimu ya afya kwa umma na waratibu wa mradi wa M- Mama kupeleka fedha kwenye akaunti ya Taifa ya M-Mama ili kufanikisha utekelezaji wa malengo kibajeti na akasisitiza kutochelewesha malipo.
"Hakuna kitu kinanikera kama kuona kifo cha mama na mtoto katika kazi zangu, pamoja na makusanyo bora ya mapato ya ndani kutokana na huduma za afya kipaumbele changu kingine ni kuona hakuna vifo vya mama na mtoto, naomba tushirikiane kufanikisha haya," amesisitiza Mganga Mkuu.
Aidha, amewataka wataalamu hao kuhamasisha jamii kuweza kutumia huduma hiyo kwa manufaa hususani matumizi sahihi ya namba ya dharula 115 kwa jamii ili isitumike vibaya badala yake waitumie kwa ajili ya kuomba msaada tu pale unapohitajika usafiri kwa mama au mtoto mchanga.
Vilevile, amesisitiza umuhimu wa kutoa mrejesho wa utekelezaji wa mpango kazi na katika hilo amewataka kufuata sheria, kanuni na taratibu za afya ikiwemo na utoaji huduma bora kwa wananchi na kwa staha ili kujenga imani kwa jamii dhidi ya Serikali juu ya huduma za afya hususani zilivyoboreshwa.
Wakati akiwasilisha mada, mwezeshaji kutoka Hospitali ya Mkoa wa Arusha (Mount Meru) Bi. Shubila Mujwahuzi alibainisha malengo ya mradi huo kuwa ni kupunguza vifo vya wajawazito na watoto ili kuimarisha rufaa kwa kuanzisha pia vyumba maalumu wagonjwa wa dharula.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.