WAFANYABIASHARA WALIOPISHA UJENZI SOKO LA MJINI KATI WATAPEWA KIPAUMBELE - RC MTANDA
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amewaahidi wafanyabiashara 802 walioondolewa mwaka 2019 kupisha ujenzi wa Soko Kuu la Mjini Kati kupata vizimba na vibanda kwenye soko jipya hivi karibuni kufuatia kukamilika kwake hadi sasa.
Ametoa kauli hiyo leo tarehe 27 Februari, 2025 alipokutana na wafanyabiashara hao pamoja na uongozi wa Wilaya ya Nyamagana katika ukumbi wa Ofisi yake kufuatia upotoshaji kuwa vibanda vya soko hilo la kisasa vimegawiwa kwa wengine.
Mhe. Mtanda amesema amebaini ya kwamba kuna baadhi ya watumishi kutoka ofisi ya Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza wamekua wakiwalaghai wafanyabiashara wapya kuwa watawapa fursa na kujipatia fedha kinyume na utararibu.
Ameongeza kuwa ugawaji wa vibanda na vizimba kwenye soko jipya unafanyika kwa kushirikiana na viongozi wa soko hilo kwa kuwabaini wale wote wenye Ilani halali na halisi walizokabidhiwa wakati wa kupisha mradi na kwamba wengine wenye ilani bandia watachukuliwa hatua pamoja na waliowapatia.
Mkurugenzi wa Halmashauri Jiji la Mwanza Wakili Kiomon Kibamba amesema soko lina nafasi 1365 na kwamba wafanyabiashara 802 walioondolewa ndiyo watakaopewa maeneo kwanza na ndipo maeneo 555 waendeleee na mchakato mwingine wa kisheria wa kuyauza.
"Hakuna mfanyabiashara mwenye ilani halisi katika wale 802 atakayekosa eneo la biashara na kwa sasa kamilisheni tu utaratibu kwa wale ambao hawana leseni za biashara ili kukidhi matakwa ya kisheria." Mkurugenzi Kibamba.
Naye, Mwenyekiti wa Soko hilo Hamad Mchola amebainisha kuwa mwezi Septemba 2019 kwa kushirikiana na uongozi wa halmashauri ya jiji la Mwanza walipisha ujenzi wa soko la mjini kati kwa ahadi ya kurejeshwa mara ujenzi utakapokamilika.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.