Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imedhamiria kukomesha uharifu na unyang’anyi ndani ya ziwa victoria kwa nunua boti 11 za doria zenye thamani ya shilingi bilioni 4.5 huku Mkoa wa Mwanza ikipatiwa boti moja ambayo imegharimu shilingi milioni 400.
Akizungumza katika tukio la ushushwaji wa boti ya doria katika ziwa victoria Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amesema Serikali inaendelea kuhakikisha inaimarisha usalama wa raia, mipaka, na mali za raia na Serikali itaendelea kufanya hivyo siku kwa siku.
Mkuu wa Mkoa amesema Mkoani Mwanza Serikali inajenga kituo kikubwa cha Utafutaji na Uokozi ndani ya Ziwa Victoria, ambapo kutakuwa na mtambo mkubwa wa mawasiliano utakaorahisisha mawasiliano ndani ya ziwa ikiwa ni mkakati unaotekelezwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki na muendelezo wa kuimarisha usalama ndani ya ziwa.
Mhe. Mtanda ameendelea kwa kusema serikali pia imenunua drone au ndege kubwa ambayo ina uwezo wa kuona sehemu kubwa ya ziwa na kubaini shughuli zote zinazoendelea ndani ya ziwa na vyombo hivyo vyote ni mali ya serikali na serikali ni moja.
“Lakini pia mnakumbuka tulileta ambulance boti kubwa kabisa, hivi vyote vitashirikiana kwa pamoja kufanya uokozi wa watu na mali zao ndani ya ziwa na mipaka yake”.
Naye, Mkuu wa Kikosi cha wanamaji Tanzania SACP Moshi N. Sokoro amesema boti hiyo ina vifaa vya kuongozea meli na mawasiliano na ni boti ambayo ina kasi sana, itahitaji utunzaji, awali amesema wamefanya mafunzo ya siku 2 kwa kuwa vifaa vilivyoletwa ni vya kisasa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza DCP Wilbroad Mutafungwa amesema kuendelea kupokea vifaa hivyo ni ishara kwamba uhalifu unakwenda kuisha kabisa kwa kuwa zitafanywa doria nyingi kwani vifaa wanavyo.
“Nitoe wito kwa wavuvi haramu na wanyang’anyi wanaofanya uhalifu ndani ya ziwa victoria waanze kutafuta shughuli nyingine za kufanya, wawaache wavuvi wafanye shuguli zao na wale wa vizimba wafanye kwa amani”. Amesema DCP Mutafungwa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.