Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Adam Malima amewataka wahandisi na maafisa manunuzi wa halmashauri kutekeleza miradi ya ujenzi kwa kuzingatia sheria ya usimamizi wa fedha za umma, manunuzi fedha za serikali za mitaa na bajeti.
Agizo hilo la Mhe. Malima limetolewa Mei 4, 2023 jijini hapa na Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Amina Makilagi kwa niaba yake alipokuwa akisoma hotuba ya kufunga mafunzo ya kuwajengea uwezo wahandisi wa mikoa na halmashauri pamoja na maafisa manunuzi kuhusu usimamizi wa ujenzi wa miundombinu ya shule za elimu ya awali na msingi kupitia mradi wa BOOST.
“Ili kupata thamani ya fedha na kuepuka hoja za ukaguzi mnapotekeleza miradi ya ujenzi zingatieni sheria, kanuni na miongozo, kama mnavyojua mradi wa BOOST ni lipa kwa matokeo sasa ili mradi huo uweze kufanikiwa na kuwa na tija tunawategemea sana nyie kufanya kazi kwa weledi, mkizingatia taratibu na maelekezo yote na kutimiza masharti na vigeo vya uhakiki vitakavyotumiwa na Wakala Huru wa Uhakiki”amesema Mhe. Makilagi.
Mhe. Makilagi ameongeza kuwa serikali inatarajia kujenga jumla ya vyumba 12,000 vya madarasa katika kipindi cha miaka mitano ya utekelezaji wa mradi wa BOOST kwa kuanzia mwaka wa pili wa utekelezaji wa mradi huo wastani wa vyumba 3,000 vitajengwa.
“Nyie tunawategemea sana katika kutekeleza miradi nawasihi msibadilishe maeneo ambayo yatapangwa kujengwa shule au ukarabati wa miundombinu maana Ofisi ya Rais TAMISEMI ilishafanya tathmini ya ujenzi wa shule na ukarabati wa mindombinu chakavu maeneo yatakayopewa kipaumbele ni yenye msongamano mkubwa wa wanafunzi, vijiji vyenye ukosefu wa shule, maeneo ambayo wanafunzi wanatembea umbali mrefu na shule za msingi zilizobainika kuwa na uchakavu mkubwa,”amefafanua Mhe. Makilagi na kuongeza
“Endapo kuna uhitaji huo halmashauri inapaswa kuwasilisha maombi hayo kwa Katibu Ofisi ya Rais TAMISEMI kupitia kwa Katibu Tawala wa mkoa ili kupata idhini hiyo,”ameeleza Mhe. Makilagi.
Aidha Mhe. Makilagi amempongeza Rais Mhe. Dk. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake za dhati katika kuondoa kero za ufundishaji na ujifunzaji shuleni ambapo ametoa fedha zaidi ya Sh bilioni 230 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu mbalimbali katika shule 1,338 za msingi zilizopo katika mikoa na halmashauri zote nchini .
“Rai yangu kwenu washiriki wa mafunzo haya imarisheni ushirikiano ngazi ya halmashauri pia tekelezeni ujenzi wa miundombinu kwa wakati na kwa ubora mkisimamia ujenzi wa miundombinu hiyo kwa weledi na uadilifu pia epukeni migogoro ambayo huchangia kucheleweshwa utekelezaji wa miradi,” Mhe. Makilagi amewaasa wahandisi hao pamoja na maafisa manunuzi.
Awali Mratibu wa Mradi wa BOOST OR- TAMISEMI, Joel Mhoja alimwambia Mhe. Makilagi kwamba mafunzo hayo yamewakutanisha washiriki 192 kutoka mikoa mbalimbali nchini lengo likiwa ni kuwajengea uwezo ili wawe na nafasi ya kusimamia vizuri utekelezaji wa ujenzi wa miundombinu kupitia mradi huo.
“Washiriki wa mafunzo haya yaliyofanyika kwa siku mbili mkoani hapa wamejengewa uwezo juu ya ramani za mpangilio wa majengo na mapitio yake, utambulisho wa DLI na vigezo vya uhakiki, usalama wa mazingira, tafsiri rasmi ya taratibu za manunuzi na utunzaji wa kumbukumbu za manunuzi,”alisema Mhoja.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.