Kamati ya Bunge ya Mazingira, Uhifadhi wa Maliasili na Usalama wa Nyuklia kutoka Ujerumani imeeleza kufurahishwa kwake na namna miradi inayofadhiliwa kwa ushirikiano baina ya Tanzania na Ujerumani inavyotekelezwa.
Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge la Ujerumani, Mhe. Sylvia Kotting-Uhl wakati wa ziara ya Kamati yake Jijini Mwanza Oktoba 4, 2019 iliyolenga kutembelea miradi ya maji iliyotekelezwa kwa ushirikiano baina ya Tanzania na Ujerumani.
Aliipongeza Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa jitihada na dhamira ya dhati iliyoonyesha kwenye kuwahudumia wananchi wake na alimuhakikishia Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. John Mongela kuwa Serikali ya Ujerumani itaendelea kuuenzi ushirikiano huo.
Mara baada ya kutembelea miradi hiyo, Mwenyekiti huyo wa Kamati ya Bunge la Ujerumani alisema kamati yake imeridhishwa na ilichokiona na alisisitiza kuwa ushirikiano uliyopo baina ya nchi hizo mbili utaendelea.
Awali kabla ya kuwasili Jijini Mwanza, Ujumbe wa Kamati hiyo ya Ujerumani ulitembelea eneo la chanzo cha maji cha mradi wa Simiyu Climate Resilience unaotekelezwa Wilayani Busega, Mkoani Simiyu.
Ikumbukwe kuwa Serikali inatekeleza mradi wa maji wa kimkakati Mkoani Simiyu utakaonufaisha zaidi ya wananchi 800,000 ambao utagharimu zaidi ya shilingi bilioni 400 kwa kutumia maji kutoka Ziwa Victoria kwa lengo la kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
Mradi huo wa Simiyu utanufaisha Wilaya zote za Mkoa huo na unatekelezwa kwa ushirikiano chini ya ufadhili wa Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Maji na Serikali ya Ujerumani kupitia Benki yake ya Maendeleo ya KfW na Mfuko wa Kijani wa Tabianchi (GCF).
Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso akiwa ameambatana na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga waliongozana na Kamati hiyo ya Bunge ya Mazingira, Uhifadhi wa Maliasili na Usalama wa Nyuklia kutoka Ujerumani na walihitimisha ziara yao kwa kutembelea miradi ya majisafi na usafi wa mazingira (majitaka) Jijini Mwanza.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.