WAKANDARASI WASIOKAMILISHA KAZI KWA WAKATI WASIPEWE ZABUNI-RAS MWANZA
Katibu Tawala wa mkoa wa Mwanza Ndugu Balandya Elikana ametoa maagizo kwa Meneja wa Tarura wilayani Ukerewe kusimamia usiku na mchana ujenzi wa barabara ya RTC-Sungura ya km 0.62 inayotekelezwa na Mkandarasi Deep Construction Ltd kwa gharama ya zaidi ya shs milioni 400 kutokana na kuwa nyuma ya muda hadi sasa.
Balandya ameagiza pia wakandarasi wanaoonesha ubabaishaji wa kutekeleza miradi ya Serikali wasipewe zabuni au kusitisha mikataba waliyokubaliana kutokana na kurudisha nyuma kasi ya kuwaletea maendeleo wananchi.
"Sijalidhishwa hata kidogo na ujenzi wa barabara hii licha ya maelekezo niliyopatiwa,kazi ya miezi sita bado iko nyuma zaidi ya miezi tisa na fedha zimelipwa hii haikubaliki,"Katibu Tawala Mkoa.
Mtendaji huyo wa Mkoa amebainisha hayo leo Septemba 17,2024 wakati akiendelea na zoezi la ukaguzi wa miradi na kusisitiza Serikali inapenda kujenga uchumi wa nchi kwa kuwashirikisha watanzania wenyewe lakini baadhi ya wakandarasi wanakatisha tamaa kwa kupewa kazi ndogo na kushindwa kuikamilisha.
"Kazi hii imeshindwa kukamilika kwa wakati kutokana na changamoto ya hali ya mvua na jiografia ya wilaya hii maji yapo juu sana kutoka ardhini na tumeomba muda hadi mwishoni mwa Novemba mwaka huu,"Reuben Muyungi,Meneja Tarura,Ukerewe
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe Mhe.Christopher Ngubiagai amebainisha maelekezo yote watayazingatia na wamejipanga kuhakikisha ujenzi huo unakamilika Novemba hii.
"Hizi ni fedha kutoka Serikali kuu na tayari zaidi ya shs milioni 165 zilizoombwa zipo mbioni kulipwa,sisi kama viongozi tuna wajibu wa kuzisimamia ipasavyo,"Mkuu wa Wilaya.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.