Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe Mhandisi Robert Gabriel leo juni 09, 2022 amefanya ziara Wilayani Sengerema na kufurahishwa na Ujenzi wa Kituo kipya cha Afya Ngomamtimba-Chifunfu kwa thamani ya Tshs. Milioni 500 ambacho utekelezaji wake utasaidia kuboresha huduma kwa wakaazi 31664 kutoka vijiji vya Chifunfu, Lukumbi na Nyakahako wanaohudumiwa na Zahanati kwa sasa.
Akikagua Mradi huo, Mhe Mkuu wa Mkoa amewataka viongozi wa Wilaya hiyo kusimamia kwa karibu ujenzi wa majengo ya Wodi ya Wazazi, njia za kutembelea, Chumba cha Upasuaji pamoja na eneo la kufulia ili kukamilisha kwa haraka lakini kwa kuzingatia ubora unaokubalika.
Aidha, Mhe Mkuu wa Mkoa amepokea taarifa ya Miradi ya kampeni ya Lishe wenye Tshs. Milioni 13, Ziro Malaria, Madawa ya Kulevya na VVU/UKIMWI ambapo ameagiza elimu ya kina kwenye maeneo hayo ili kuhakikisha afya bora kwenye jamii na kukomesha utapiamlo kwa watoto, mazalia ya Mbu pamoja na tabia hatarishi hasa kwa vijana.
"Pamoja na kupewa mkopo ni haki yao kupewa mafunzo ili kufanya kikundi kuwa hai na chenye heshma kwa wenzao wanaowazunguka," amesisitiza Mkuu wa Mkoa wakati akikagua kikundi cha Vijana watengeneza Mitumbwi Kijiweni waliokopeshwa Tshs Milioni 5 na Halmashauri.
Awali, Meneja RUWASA Wilaya ya Sengerema aliufikisha msafara wa Mhe. Mkuu wa Mkoa kwenye Mradi wa Maji ya bomba wa Mwaliga-Nyamahona-Kasenyi ambao umegharimu Tshs Milioni 700 ukihudumia wananchi kwenye Vijijini vitatu vya kata ya Kasenyi huku ukiwa na vituo 16 vya kuchotea maji.
"Lengo la kufika hapa ni kuona thamani ya Mradi huu na kuhakikisha Mali ya umma hailiwi kwani Serikali imewaletea wananchi fedha za Miradi ili kuboresha maisha yao na sio kuwaletea watu wachache wale." Amesema, Mhe Mkuu wa Mkoa akitoa rai kwa viongozi na wananchi kutunza mradi.
Vyumba 4 vya Madarasa vilivyojengwa chini ya Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Uviko 19 kwa Tshs Milioni 79.3 vimemfikisha Mhe Mkuu wa Mkoa kwenye Shule ya Sekondari Katunguru ambapo baada ya kukagua ametoa wito kwa uongozi wa shule hiyo kuondoa dosari ndogo zilizobainika ili yawe nadhifu.
Kwa bajeti ya Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo, Tshs milioni 31.7 zimejenga barabara ya DM Petrol Station- Sengerema DDH yenye KM 1.9 ambapo baada ya Mkuu wa Mkoa kuikagua ameagiza uwekwaji wa mitaro ambayo itachepusha maji machafu na kusaidia kulinda uiamara wa Barabara.
"Tunawapongeza uwekezaji mzuri na wananchi watapata huduma ila hakikisheni masuala ya usalama yanazingatiwa maana kikitokea kitu halafu msijue nini kifanyike hamtakua salama." Mkuu wa Mkoa akikagua Kituo cha kuuzia Mafuta cha Silya Oil kilicho mtaa wa Ibisabageni kilichogharimu Tshs Milioni 372.5.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.