Wakati zoezi la Sensa ya Watu na Makazi likitarajiwa kuanza Agosti 23 mwaka huu wakazi wa Mkoani Mwanza wameonesha mwitikio chanya hali inayoonesha zoezi hilo litafanyika kwa ubora uliokusudiwa.
Mary Marco miongoni mwa Makarani wa Sensa Wilaya ya Ilemela aliyefanya zoezi la uwandani lililofanyika leo Agosti 11,2022, amesema kaya nyingi walizotembelea wameonesha uelewa na ushirikiano.
"Nimetembelea baadhi ya kaya eneo la kata ya Kawekamo sikupata changamoto yoyote maswali niliyouliza nimejibiwa kwa usahihi" Karani wa Sensa.
Ameongeza kuwa, zoezi la uwandani ambalo ni la vitendo limehusisha kutambua mipaka ya kila eneo la Karani wa Sensa litakalohusisha Kaya 100.
Naye Mwenyekiti wa Kituo cha Mafunzo Butimba Wilayani Nyamagana Innocent Muyaja amesema zoezi la uwandani ni la siku moja na baada ya hapo Makarani wa Sensa wanarudi mafunzoni kuzungumzia changamoto walizobaini na kuzifanyia kazi.
Aidha Muyaja amefafanua kuwa, mafunzo kwa Makarani hao yanakwenda vizuri hasa uelewa mzuri wa wahusika kwa Madodoso yote manne ya Sensa,Jamii,Makundi Maalum na Majengo.
Sensa ya Watu na Makazi itafanyika nchi nzima kwa watu waliopo ndani ya mipaka ya Tanzania Agosti 23 mwaka huu.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.