Naibu Waziri wa kilimo Hussein Bashe amewatahadharisha wale waliohusika na upotevu wa fedha shilling billion 123 za wakulima kupitia kwenye vyama vya ushirika vya kilimo na masoko ( AMCOS) watachukuliwa hatua za kisheria ili kuurudisha ushirika huo katika mstari na kuhakikisha haki ya mkulima inalindwa.
Hayo yalibainishwa na Naibu Waziri wa kilimo Hussein Bashe wakati wa mkutano wa 16 wa wadau wa sekta ndogo ya pamba Tanzania uliowakutanisha wakulima, wakuu wa wilaya, wakuu wa mikoa, wakurugenzi, wabunge na viongozi vyama vya ushirika kutoka mikoa 17 ya Tanzania bara inayolima zao la pamba , uliofanyika jijini hapa lengo likiwa kuongeza tija katika zao hilo hivyo alisema hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa wale waliohusika na upotevu wa fedha hizo.
" Hili hatutalifumbia macho kwa sababu hakuna watu wanaowaibia wakulima kama vyama vya ushirika vya kilimo na masoko (AMCOS ) kwa mujibu wa wakaguzi wa mahesabu ya ndani (COASCO ) kuna upotevu wa fedha za wakulima billion 123 kupitia AMCOS hivyo wale wote waliohusika lazima watachukuliwa hatua " alisema Bashe.
Pia aliitaka bodi ya pamba nchini kujizatiti na kuimarisha ushirika ili mkulima aweze kuzalisha zao hilo kwa bei ndogo ili aweze kupata tija ya kilimo hicho kwani sekta ya pamba ni nzuri kama utakuwepo muungano wa ushirika utakaofanya mageuzi makubwa hivyo serikali inalenga kuwekeza katika uzalishaji wa mbegu.
Alisema kilimo ni biashara hivyo ni vyema misingi yake iheshimiwe suala la mbegu tayari linashughulikiwa lakini serikali haitakuwa tayari kupewa masharti yasiyokuwa na maslahii kwa Taifa kutoka kwa wafadhili wa nje.
" Serikali itasaidia kupunguza gharama za uzalishaji kwa wakulima na kuwajengea njia nzuri ili wasipate hasara na haitaingilia suala ya bei ya pamba ila soko ndio litakaloamua " alisema Bashe.
Aliongeza kuwa mkopo wa mabenki nchini ni Trillion 16 asilimia nane tu ndiyo inaenda kwenye kilimo, pia sekta ya kilimo haikopesheki kutokana kutokuwa na dhamana hivyo serikali imeamua kutafuta fedha na kuipatia benki ya maendeleo ya kilimo (TADB) ili ichukuwe dhamana ya kuwakopesha wakulima na imeanza mazungumzo na taasisi za kifedha za kimataifa zitakazoipatia fedha benki hiyo ili iwe na uwezo wa kukopesha wakulima ambapo hivi sasa washapatiwa billion 40.
Awali ya yote akitoa salamu na kumkaribisha mgeni rasmi kufungua mkutano huo wenye kauli mbiu ya wekeza kwenye tija kuongeza kipato cha mkulima na kufikia uchumi wa viwanda Mwenyekiti wa balaza la wakurugenzi bodi ya pamba Joe Kabisa alisema hatari iliyopo sasa katika kilimo cha zao hilo ni uwepo wa funza wekundu hivyo harakati za haraka zinaitajika ili kuwadhibiti ili kuwa na maendeleo endelevu ya sekta hiyo nchini.
Aliongeza kuwa kutokuaminiana ndani ya sekta ni changamoto kubwa inayowakabili hivyo ushirikiano wahitajika ili kusonga mbele pia alimuomba Naibu waziri Bashe kuimarisha mfuko wa pamba unaowezesha upatikanaji wa pembejeo.
Naye Mkurugenzi wa bodi ya pamba Marco Mtunga alisema changamoto muhimu zinazolikabili zao la pamba ni kukosekana kwa uhakika wa upatikanaji wa pembejeo bora zikiwemo mbegu, viuatilifu, mbolea vinyunyizi, utoaji hafifu wa huduma za ugani na matumizi ya zana duni za kilimo hivyo vinachangia tija duni na ubora hafifu.
Dkt Charles Tizeba aliyekuwa Waziri wa Kilimo , Umwagiliaji na Ushirika, Agrey Mwanri Mkuu wa Mkoa wa Tabora na Mohammed Yahaya Mkulima ni baadhi ya washiriki wa mkutano huo walisema elimu inayohitajika na yenye maslah kwa taifa ni ya uzalishaji wa zao la pamba .
Pia ili kuwa na uendelevu wa uzalishaji , serikali iachie mazao makubwa likiwemo zao la pamba yajiendeshe pasipo kutegemea ruzuku ya serikali.
" Uboreshwaji wa viuatilifu uzingatiwe kwa sababu imegeuka changamoto kwa sisi wakulima tunapulizia kwenye mazao yetu lakini mdudu asife na kusababisha tupate hasara"alisema Yahaya.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.