*Wamiliki wa Biashara za Vileo watakiwa kuzingatia Sheria na Kanuni za Uendeshaji Biashara**
Katika kuhakikisha kwamba biashara za Vileo zinafanyika kwa amani na utulivu, Wamiliki wa Biashara hizo wametakiwa kuzingatia Sheria na Kanuni za uendeshaji wa biashara hizo kwani kwa kukiuka kufanya hivyo na kuzalisha kelele sumbufu, watachukuliwa hatua kwa mujibu wa taratibu za Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira NEMC.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Wilaya ya llemela Mhe.Hassan Masalla, akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza leo Mai 22, 2023 katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, alipokutana na Vyombo vya Habari.
Mhe.Hassan Masalla amebainisha kuwa Mkoa wa Mwanza kwa kushirikiana na NEMC Mei 5, 2023 walifanya zoezi maalum la kaguzi 50 za wafanyabishara za Vileo na kubaini maeneo 31 ya biashara za vileo kwenda kinyume na Sheria na kuchukuliwa hatua na kupewa maelekezo namna ya kudhibiti kelele hizo sumbufu.
"Ndugu zangu waandishi nawaomba muwaelimishe vyema wananchi kuhusiana na Sheria na Kanuni za kudhibiti kelele sumbufu, baadhi yetu tumekuwa siyo rafiki na hali hii kutokana na sababu mbalimbali, Serikali inaheshimu taratibu zote zilizowekwa, Biashara hizi zilizobainika kukiuka Sheria zimepigwa faini kati ya Milioni 2 hadi 5 huku zikiendelea kutoa huduma nyingine kama kawaida," amefafanua Mhe.Masalla.
Aidha, amebainisha kuwa maeneo ya biashara za vileo zilizotozwa faini ya Shilingi Milioni 5 ni zile zilizobainika kuwa sugu kwa kuzalisha kelele sumbufu licha ya kuonywa mara kadhaa,na sasa zimetakiwa kuweka vifaa maalum vya kudhibiti kelele hizo.
"Tumejitahidi kuwapa ellimu ya kutosha licha ya kuwapa adhabu kwa mujibu wa kanuni zetu,tunashukuru sasa wamepata uelewa mzuri ili mwisho wa siku kusiwepo na kero kati ya anaye starehe na aliyepo nje na eneo la starehe,"Jerome Kayombo,Meneja Mkoa NEMC.
Aidha Mhe.Masalla amesema zoezi la ukaguzi wa nyumba za ibada litafuata baada ya kukamilika taratibu maalum kwani siyo rahisi kufanya kwa pamoja kaguzi za sehemu za vileo na nyumba za ibada.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.