Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Mhandisi Robert Gabriel anaendelea na Kampeni ya Ujenzi wa Miundombinu ya Madarasa ambapo leo ameungana na maelfu ya wananchi na wadau kuchimba Msingi wa Madarasa 44 katika shule ya Msingi Bujora wilayani Magu.
Akizungumza na wananchi hao walioshiriki uchimbaji wa Msingi kwenye shule hiyo amewapongeza kwa kuonesha kiu ya kujiletea maendeleo na amebainisha kwa kujitolea huko ni dhahiri wanamuunga mkono Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa vitendo.
"Maendeleo ya wananchi wa Mwanza yataletwa na wanaMwanza wenyewe, hongereni na Mungu awabariki sana kwa jambo hili kubwa mlilofanya na msiache tabia hii njema kwani desturi ya kutoa inatupa heshma sana na hadhi hata mbele za Mungu kwani kutoa ni moyo na sio kwa sababu ya kuwa unavyo vingi bali ni kwa upendo kwa watoto wetu." Mkuu wa Mkoa.
Mkuu wa Wilaya ya Magu Mhe. Salum Kali amewashukuru wananchi waliojitokeza kwa hamasa kubwa kuchangia nguvu kazi kwenye kampeni ya Ujenzi wa Madarasa na ametumia wasaa huo kuwakumbusha kujiandaa kushiriki zoezi la Sensa ya watu na Makazi itakayofanyika Agosti 23, 2022.
"Namshkuru sana ndugu yetu Mkuu wa Mkoa kwa kazi anayofanya akishirikiana na viongozi wenzake nasema mnakitendea haki Chama Cha Mapinduzi kupitia Ilani, sisi kama wasimamizi tunaridhishwa na Maendeleo haya." Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Magu.
"Nimetoa matofali 400 kwa ajili ya watoto wetu nawaomba tumuunge mkono Mhe. Rais Mama Samia kwani anatujali sana wananchi wa Mkoa wa Mwanza na ndio maana mnaona anatufanyia mengi kwenye kila sekta." Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Mwanza Mhe. Kabula Shitobelo.
"Hapa vinahitajika vyumba 44 na watoto hawa ni wetu wote ila hata mwalimu akiwa na uwezo namna gani hawezi kufundisha wanafunzi 175 ndani ya darasa moja hivyo tuendelee kuchangia nguvu kazi, nami pamoja na matofali ya Mhe Mbunge wa viti Maalum nitahakikisha yanaletwa matofali 2000 hapa leo hii." Mhe. Kiswaga Deus, Mbunge Magu.
"Wanabujora mmepata bahati kiwilaya, Mhe Mkuu wa Mkoa tunakushuruku sana tunahitaji viongozi kama ninyi ambao mnatambua changamoto za wananchi wa chini na kuwasaidia, sisi kama Halmashauri tunapeleka fedha kwenye miradi hii kwa ajili yakuikamilisha." Mhe. Simon Mpandalume, Mwenyekiti Halmashauri ya Magu.
"Mimi kama mwenyekiti wa Kitongoji hiki natoa matofali 800 kwenye Ujenzi huu maana nilifurahishwa sana niliposikia kuwa Mkuu wa Mkoa atakuja hapa kuanzisha ujenzi wa Madarasa na nilisema kwakweli ni jambo jema na sitamuangusha," amesema Mhe. Doto Mtimkavu.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.