WANANCHI TUMIENI KAMBI YA MADAKTARI SEKOU TOURE KUPATA MATIBABU YA KIBINGWA : RAS BALANDYA
*Awapongeza Seko Toure kwa kutoa nafasi ya matibabu kwa wananchi*
*Asema kambi ya Madaktari itazidi kuitangaza Hospitali ya Sekou Toure*
*Akiri Magonjwa yasiyoambukiza bado ni tatizo kwa wananchi wengi*
Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Balandya Elikana leo Machi 4, 2024 amezindua kambi ya Matibabu ya kibingwa kwa muda wa siku nne kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Seko Toure.
Akizungumza na wananchi waliofika kwa matibabu hayo, Balandya amesema hiyo ni fursa ambayo wananchi wanatakiwa kuichangamkia hasa kutokana na ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza kama kisukari na shinikizo la damu.
Akiambatana kujionea shughuli za kitabibu na Mganga Mkuu wa Mkoa Thomas Rutachunzibwa na Mganga Mfawidhi wa Sekou Toure Bahati Msaki Balandya amebainisha kuwa wananchi wanaofika watazidi kufahamu huduma mbalimbali za kibingwa zinazotolewa hospitalini hapo ikiwemo usafishaji wa damu.
"Hospitali hii ilianza mwaka 1964 ikiwa ni kitengo cha wagonjwa wa nje na mwaka 2010 ikapewa hadhi ya kuwa Hospitali ya rufaa na imekuwa ikipiga hatua na sasa inatoa huduma za kibingwa", Katibu Tawala Mkoa.
"Kwa muda wa kambi hii itawahudumia wananchi wenye bima na wale wasio na bima watapatiwa matibabu kwa bei nafuu na upimaji wa magonjwa ya sukari, Shinikizo la damu, Saratani ya Matiti na Shingo ya uzazi huku VVU hakutakuwa na malipo," Dkt. Rutachunzibwa.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Sekou Toure Bahati Msaki ameishukuru Serikali ya Rais Samia kwa kuendelea kuiboresha kihuduma taasisi hiyo kiasi cha kutoa huduma kwa idadi kubwa ya wananchi
"Mwaka 2014 tulikuwa na wagonjwa 155,718 kwa mwaka na kufikia 246, 627 mwaka 2015 hii ikatulazimu kujenga jengo jipya la mama na mtoto", amefafanua Mganga Mfawidhi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.