Wananchi wa Kijiji cha Chasarawi katika Kata ya Bupamwa wilayani Kwimba wamechangishana na kununua eneo la ardhi lenye ukubwa wa Hekari nane kwa ajili ya kujenga Shule ya Msingi ili kuwapunguzia watoto adha ya kutembea umbali mrefu wa zaidi ya Kilomita tano.
Hayo yamebainishwa leo wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe Adam Malima ambapo kiongozi huyo amekagua na kuweka Jiwe la Msingi kwenye ujenzi wa Miundombinu ya vyumba vya Madarasa 9, Matundu ya Vyoo 30 na Jengo la Utawala kwenyw shule ya Msingi Mwalulyeho yanayotekelezwa kwa Tshs. Milioni 150 zilizotolewa na serikali kuu.
Amesema, wananchi wa kijiji hicho wameonesha kuwa na kiu ya maendeleo na uzalendo kwa kuamua kwa hiyari kununua eneo na kuanzisha ujenzi kabla ya serikali kuwaletea mawazo na akatumia wasaa huo kuwaahidi kuwatimizia ndoto yao ya kupata shule kwa kuhakikishia kukamilika kwa ujenzi mapema mwezi Aprili 2023.
"Nawashukuru sana kwa kujitolea kuanzisha mradi wa maendeleo na ukiona jamii inafanya haya kwa hiyari basi ujue eneo hilo wananchi wake wanajitambua sana maana hakuna mtu anayeweza kujenga shule ili asome mwanae pekee bali ni kwa ajili ya jamii nzima., hongereni sana." Malima.
Aidha, ametoa rai kwa wazazi wa kata ya Bupamwa kuhakikisha wanawapeleka watoto shule hususani wa kike ili kuwatimizia ndoto ya kujitegemea na akawasihi kuacha tabia ya kuwaozesha kwa kishawishi cha kupata mifugo kama mahari huku akisema wakifanya hivyo wataharibu jamii nzima ya sasa na baadae.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Kwimba Mhe. Ngw'ilabuzu Ludigija ametumia wasaa huo kumshukuru Mhe Rais kwa kuwaletea fedha za ujenzi wa shule hiyo na akawapa kongole wananchi kwa kuamua kujiletea maendeleo wenyewe bila kusubiri na akawataka kuendelea na tabia hiyo njema.
"Rais Samia hakukosea kukuleta Mhe. Malima Mkoani Mwanza maana tutanufaika sana na Uongozi wako maana una uchungu wa maendeleo ndio maana pamoja na kufanya ziara za kusikiliza kero za wananchi unahakikisha unakagua kila mradi hadi iliyopo maeneo ya mbali kiasi hiki." Me. Sabana Salinje, Mwenyekiti wa CCM Magu.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kwimba Mhe. Thereza Luhangija amewapongeza wananchi kwa kujitolea kuanzisha mradi huo kwa kiu ya maendeleo yao wenyewe na akatoa wito kwao kutunza miundombinu hiyo ili iwasaidie vizazi vya sasa na baadae.
Awali, Mhe. Mkuu wa Mkoa amefika kwenye kata ya Mwamitinje na kukagua Ujenzi wa vyumba 3 vya madarasa na matundu 6 ya vyoo kwa zaidi ya Tshs. Milioni 84 chini ya mradi wa kupunguza umasikini (TASAF) na akawasihi kamati ya Ujenzi kufanya kazi hiyo kizalendo na yeyote atakayehujumu ujenzi huo atachukuliwa hatua kali za kisheria.
Hata hivyo, Mkuu wa Mkoa akiwa eneo la hifadhi ya Maji ya Bonde Kwimba, ameagiza ufanyike utambuzi na uhakiki wa mipaka ili kupata suluhu ya mgogoro kati ya wananchi na Mamlaka ya bonde la ziwa Victoria.
Amesema timu ya Mkoa, Bonde la Maji ya ziwa Victoria na Halmashauri watakuja na ramani ya mwaka 1958 ili kujiridhisha kama wananchi wanaodai kuporwa ardhi yao wako ndani ya hifadhi ama laa na amewataka waje na wataalam wa ramani ili wasije kudai kuwa walilazimishwa.
Katika nyakati tofauti Mhe Mkuu wa Mkoa ameziagiza RUWASA, TANESCO, REA kupeleka huduma kwenye miradi ya VETA inayotarajia kuanza Julai mwaka huu, Kituo cha Afya Hungumarwa ambacho amekizindua rasmi kwa ajili ya kuanza kutoa huduma mwezi Aprili.
Kabla ya kuhitimisha ziara kwa kuzindua mradi wa Maji wenye thamani ya Milioni 650 kwenye kijiji cha Ngula na kuwataka wananchi kuutunza,ziara ya Mhe. Malima imemfikisha kwenye Shamba la Hekari 2.5 la bwana Gogomoka Mkonongo lililopo kwenye kijiji cha Ligembe ambaye amepanda kitaalamu kwa kufuata sheria bora za kilimo huku akiwa akitumia mbolea ya samadi na akawaagiza maafisa Ugani kutoa Elimu ya Kilimo bora.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.