WANANCHI WA HUNGUMALWA KWIMBA WAPATA MRADI MKUBWA WA MAJI WA ZAIDI YA BILIONI 10
*RC Makalla amshukuru Rais Samia kwa kutenga fedha zaidi ya Bilioni 10 kutekeleza mradi huo*
*Awataka wananchi kulinda miundombinu ya maji na kuumiliki mradi huo kupitia jumuiya ya watumia maji*
*Amemtaka Mkandarasi kukamilisha ujenzi wa mradi huo kwa mujibu wa mkataba*
*Awataka Kamati ya Siasa na Mkuu wa Wilaya hiyo kuendelea kufuatilia mradi huo*
*Abainisha kuwa wananchi zaidi ya elfu 24 watanufaika na mradi*
*Amewasihi wananchi kuacha kutumia maji ya Ziwa badala yake watumie maji safi na salama ya bomba*
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. CPA Amos Makalla leo Novemba 28, 2023 amekagua mradi mkubwa wa maji unaojengwa na Emirates Builders Company Ltd kwa zaidi ya Bilioni 10.8 kwenye Kata ya Hungumalwa wilayani Kwimba.
Akizungumza na wananchi baada ya ukaguzi huo CPA Makalla ametumia wasaa huo kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutenga fedha zaidi ya Bilioni 10.8 kujenga mradi huo ambao hadi sasa umetekelezwa kwa asilimia 80 huku ukikusudiwa kunufaisha zaidi ya wananchi elfu 24.
Makalla amesema akiendelea na ziara yake wilaya ya Kwimba ambayo ameianza Novemba 27, 2023 amebaini pamoja na miradi mingine kuna miradi mikubwa mitatu ya maji tena kwenye vijiji vya mbali jambo ambalo ni ishara ya adhma ya nia njema ya Serikali kuwapatia wananchi maji safi na salama.
Aidha, amewasihi wananchi kuacha tabia ya kutumia maji ya ziwa na badala yake amewataka kutumia maji safi ya bomba pamoja na kuhakikisha wanalinda miundombonu ya miradi hiyo pamoja na kuimiliki kupitia jumuiya ya watumia maji ili iweze kuwasaidia kwa muda mrefu.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi, Mkuu wa Wilaya ya Kwimba Ng'wilabuzu Ludigija amemshukuru Rais Samia kwa kuwaletea mradi huo wananchi ambao awali wamekua wakitumia maji ya ziwa yaliyowapelekea kuugua magonjwa ya tumbo na ametoa rai kuunganisha maji kwenye nyumba zao kwani ni watu 490 tu wameunganishwa.
"Mradi huu unaotumia chanzo cha bomba kuu la KASHWASA utasaidia kuwapatia wananchi wa Hungumalwa maji safi kwa asilimia 100 hususani katika kata ya Ilula ambao kwa sasa wanapata maji kwa asilimia 50 tu" Amefafanua Meneja wa RUWASA (W) Mhandisi Godliver Gwambasa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.