WANANCHI WA KATA YA KISEKE - ILEMELA WAMSHUKURU RAIS SAMIA KWA KUJENGEWA SHULE YA SEKONDARI
*Zaidi ya Milioni 584 zatumika kujenga Miundombinu ya shule hiyo Mpya*
*Itasaidia kuondoa msongamano wa wanafunzi kwenye shule Mama ya Angelina Mabula*
*Kusaidia kuondoa adha ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma ya elimu*
*RC Makalla aagiza kujengwa uzio kwenye shule hiyo*
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. CPA Amos Makalla anaendelea na ziara yake ya usikilizaji na utatuzi wa kero za wananchi pamoja na ukaguzi wa miradi ya maendeleo na mapema leo asubuhi amekagua ujenzi wa shule mpya ya Sekondari inayojengwa kwenye kata ya Kiseke wilayani Ilemela.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi Diwani wa Kata ya Kiseke Mhe. Ramadan Mwevi amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwaondolea wanafunzi adha ya kutembea umbali mrefu kufuata elimu kwenye shule mama ya Angelina Mabula kutokana na kutoa zaidi Milioni 584 kupitia mradi wa Sequip.
Mhe. Mwevi amesema kwa muda mrefu watoto wamekua wakisongamana kwenye shule ya Sekondari ya Angelina ambayo ndio shule mama lakini kwa usikivu wa Rais Samia ameamua kuwaondolea adha hiyo watoto ndipo akaleta fedha za kujenga shule hiyo mpya kabisa ambayo ipo katika hatua za mwisho kukamilika.
"Kwa niaba ya wananchi wa Kata ya Kiseke, ninamshukuru sana Mhe. Samia Suluhu Hassan Rais wetu kwa kutuletea fedha hizi kujenga shule ya Sekondari kwenye kata yetu maana tumeondokana na adha za msongamano darasani na umbali kwenda kwenye shule mama, lakini pia ujenzi huu umetoa ajira za muda kwa vijana wanaojenga na mama lishe." Mhe. Diwani.
Akizungumza kwenye ukaguzi huo, Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Mhe. Hassan Masalla amebainisha furaha yake kwa kupata mradi huo kwa kuahidi kukamilisha ujenzi ifikapo Novemba 15, 2023 ili watoto waanze kupata elimu kwenye shule hiyo mapema shule zitakapofunguliwa mwakani.
Mhe. Mkuu wa Mkoa ametumia wasaa huo kumshukuru Rais Samia kwa kuboresha huduma za elimu na akawaahiza halmashauri kuhakikisha wanalinda Miundombinu hiyo na watoto kwa kujenga uzio kuzunguka shule hiyo ambapo amebainisha kuwa utasaidia kupunguza migogoro ya ardhi.
Akikagua ujenzi wa hospitali ya wilaya ya Ilemela kwa zaidi ya Bilioni 3.4 iliyopo kwenye kata ya Sangabuye Mhe. Makalla amewataka LATRA kwa kushirikiana na Jeshi la polisi kuweka utaratibu wa daladala kufika kwenye hospitali hiyo ili kuwapunguzia wananchi gharama za usafiri wa kufika kupata huduma.
Awali akikagua maendelezo ya ujenzi wa barabara ya Nyakato (VETA)-Buswelu hadi Muhonze (KM 2.5) kipande kinachojengwa kwa Bilioni 2.9 CPA Makalla amewataka TANROADS kusimamia ubora na wananchi kulinda Miundombinu hiyo hususani taa ambazo wananchi wamekua na mtindo wa kuziiba.
Mhe. Mkuu wa Mkoa amehitimisha ziara wilayani Ilemela kwa kushiriki zoezi la kulaza bomba ardhini kama ishara ya uboreshaji mfumo wa usambazaji maji ambao utawanufaisha wananchi wa Buswelu, Kahama, Nyamadoke, Busenga, Bulela A, Zembwela na Kangae umbali wa Kilomita 49.4 kwa Bilioni 4.7.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.